Vijana wawili wauawa katika maandamano Morocco
2 Oktoba 2025
Watu hao wawili waliuawa kwa bunduki katika mji wa Leqliaa ulioko umbali wa kilomita zipatazo 500 kusini mwa mji mkuu, Rabat. Polisi walifyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji, kwa hoja kwamba hatua hiyo ilichukuliwa ili kujilinda.
Shirika la habari la serikali ya Moroko lilinukuu taarifa ya mamlaka ya eneo hilo, iliyosema kuwa watu wawili walioelezewa kuwa 'wafanya-fujo' wameuawa na polisi kwa kujihami. Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa watu hao waliuawa wakijaribu kupokonya silaha kutoka mikononi mwa polisi, ingawa hakuna ushahidi wowote uliotolewa.
Maandamano hayo dhidi ya serikali yanayoendeshwa chini ya vuguvugu lisilo na kiongozi, la vijana watumiaji wa mitandao ya kijamii, yameishitua Moroko, na yanaonekana kuwa makubwa zaidi kwa kipindi kirefu. Hadi katikati mwa wiki hii yameonekana kusambaa katika maeneo mapya, licha ya kwamba hayajapatiwa ruhusa kufanyika.
Walia na uwekezaji wa mabilioni kwenye Kombe la Dunia, ufisadi uliopitiliza
Washiriki wa vuguvugu hilo la vijana maarufu kama Gen Z wanalalamikia kile wanachokiona kama ufisadi uliopitiliza. Kupitia nyimbo na mabango, wanapinga matumizi ya mabilioni yanayowekezwa katika maandalizi ya fainali za kombe la dunia la mwaka 2030, huku shule na hospitali zikiwa katika hali mbovu kutokana na upungufu wa bajeti.
Lakini nyimbo zao zilikatizwa pale ghasia zilipoibuka katika miji mbali mbali usiku wa kuamkia wa leo, kufuatia kamata kamata iliyowazoa wengi, kwa hali ya kipekee katika mikoa ambako hali ya ukosefu wa ajira na huduma za kijamii ni mbaya zaidi.
Katika mji masikini wa Sale ulioko ng'ambo ya pili ya mto unaoutenganisha na mji mkuu, shirika la habari la Associated Press lilishuhudia mamia ya vijana waliofunika nyuso zao wakichoma moto magari, wakiharibu mabenki na maduka, huku wakivunja vioo vya madirisha na kufanya uporaji. Hakuna polisi waliokuwa wakionekana kuuzuia uhalifu huo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Discord, vuguvugu la Gen Z 212 linaloyaratibu maandamano haya liliwataka washiriki kuelezea hisia zao kwa utulivu, na kukosoa ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama.
Vuguvugu hilo lilisema kwenye taarifa hiyo, kuwa haki ya kupata huduma za afya, elimu na maisha yenye heshima, ni ya msingi na haiishii tu katika kauli mbiu.
Jumamosi iliyopita wizara ya mambo ya ndani ya Morocco ilisema kuwa maandamano hayo yasiyo na kibali yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Ilisema tayari washukiwa 409 walikuwa wametiwa mbaroni, na maafisa 263 wa usalama walikuwa wamejeruhiwa. Aidha, kwa mujibu wa wizara hiyo, magari 142 ya vyombo vya usalama yalikuwa yameharibiwa.