Maandamano ya wanawake dhidi ya Trump
22 Januari 2017Maandamano hayo yamewahamasisha wengi katika taifa hilo, na wengine zaidi ya milioni moja wakimiminika katika mitaa ya miji ya Marekani wakiandamana kwa amani. Maandamano hayo ni ishara ya awali ya upinzani mkali anaokabiliana nao rais huyo kutoka chama cha Republican.
Mamia kwa maelfu ya wanawake , wengi wakivalia kofia za rangi ya waridi , pinki kupinga matamshi ya Trump ambayo yamezusha hasira miongoni mwa wanawake, walijazana mjini Washington karibu na Ikulu ya Marekani ya White House.
Mamia kwa maelfu ya wanawake waliingia mitaani mjini New York, Los Angeles , Chicago na Boston kumdhihaki Trump katika siku yake kamili ya kuwapo madarakani.
Mkusanyiko wa watu walioandamana mjini Washington ulionekana kuwa mkubwa zaidi ya kundi lililojitokeza katika sherehe za kuapishwa kwa Trump.
Wanawake waandamana duniani kote
Duniani kote pia wanawake waliandamana wakiwaunga mkono wanawake wa Marekani na waliungana kuonesha hasira yao katika miji mingi, na kufikisha idadi ya waliohudhuria maandamano hayo kufikia zaidi ya wanawake milioni 4, wamesema watayarishaji wa maandamano hayo.
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajia kukutana na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May pamoja na rais wa Mexico Enrique ena Nieto , washirika wa muda mrefu wa Marekani hivi karibuni , wakiwa na wasi wasi juu ya vipi uongozi wake unaweza kuathiri uhusiano wao na Marekani.
Trump atakutana siku ya Ijumaa na May mjini Washington , amesema msemaji wa Ikulu ya Marekani ya White House Sean Spicer jana Jumamosi.
Mkutano wao utakuwa fursa kwa May, ambaye hapo kabla alipata taabu ya kujenga uhusiano na kikosi cha Trump cha kipindi cha mpito, kujadili kile ambacho kwa muda mrefu kilielezwa kuwa ni "uhusiano maalum" kati ya mataifa hayo mawili, nguzo muhimu ya sera za kigeni za Uingereza.
Trump aliidhinisha Uingereza kujitoa EU
Trump , ambaye aliidhinisha kura ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa ulaya na ni rafiki wa mkosoaji mkubwa wa May Nigel Farage , amesema anataka kutayarisha makubaliano ya haraka ya kibishara kati ya mataifa hayo mawili , Marekani na Uingereza.
Biashara itakuwa pia ajenda katika mkutano kati ya Trump na Pena Nieto pamoja na usalama na uhamiaji, Spicer aliwaambia waandishi habari.
Baada ya kuapishwa rais Donald Trump kuwa rais wa 45 nchini Marekani , "dunia ya kale ya karne ya 20 haipo tena," waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliandika katika makala maalum kwa ajili ya gazeti la Bild am Sonntag leo Jumapili (22.01.2017).
Vipi dunia ya kesho itakavyoonekana hilo halijaamuliwa , bado hilo liko wazi," ameongeza waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani. "Kama kawaida wakati madaraka yanatoka kutoka mkono mmoja kwenda mwingine , kunakuwa na hali ya sintofahamu, wasi wasi na maswali juu ya mwelekeo wa uongozi mpya. Lakini katika nyakati hizi za mkanganyiko mpya wa dunia, leo hii kuna mambo mengi yanayohitajika," amesema Steinmeier.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid