1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Maandamano ya Watu Milioni Moja" yaendelea Misri

1 Februari 2011

Maandamano yaliyopewa jina la "Mkusanyiko wa Watu Milioni Moja", yameanza rasmi hii leo, yakiwa muendelezo wa wiki nzima wa maandamano dhidi ya Rais Hosni Mubarak ajiuzulu, huku jamii za kiraia zikimtaka akubali haraka.

Waandamanaji katika uwanja wa Tahrir
Waandamanaji katika uwanja wa TahrirPicha: picture alliance / dpa

* Waaandamanaji wakaidi amri ya serikali

* Jeshi laapa kutokutumia nguvu kwa raia

* NGOs zamtaka Mubarak aondoke

Shinikizo dhidi ya Rais Hosni Mubarak linazidi kuongezeka, na bado haijulikani ni kwa kiasi gani kiongozi huyu ataendelea kuhimili shinikizo hili.

Hivi leo, maelfu kwa maelfu ya Wamisri wameendelea kumiminika katika mji mkuu wa Cairo, wakiitikia wito wa vuguvugu la vijana wa Aprili 6, kushiriki "Maandamano ya Watu Milioni Moja."

Serikali yaongeza marufuku ya kutotembea ovyo

Muandamanaji akishinikiza Mubarak aondokePicha: picture alliance/dpa

Serikali imeongeza muda wa marufuku ya kutotembea ovyo, iliyoanza tangu Ijumaa iliyopita, na televisheni yake imekuwa ikitoa matangazo yanayowaonya watu wabakie majumbani mwao, lakini hakuna dalili ikiwa waandamanaji wanaiheshimu tena serikali hii.

"Mubarak amekuwapo madarakani kwa miaka 30 sasa. Tulimuheshimu na kumuogopa sana. Lakini yeye hakutaka kuwa mtu mwema. Alitumia udikteta, udhalimu na ukandamizaji. Nasi sasa hatujui tena thamani ya maisha. Tumechoka; na ule moto uliojivundika nyoyoni mwetu, sasa ndio umeanza kutoka." Amesema na mmoja wa waandamanaji.

Huku helikopta za jeshi zikipita juu yao, waandamaji kwenye uwanja wa Tahrir wameendelea kupiga kelele za kumlaani Mubarak na utawala wake, na wakiapa kwamba hawataondoka hapo hadi lengo lao limetimia.

Jeshi kutokutumia nguvu

Muandamanaji akisali mbele ya askari wa MisriPicha: AP

Mwandamanaji mmoja ambaye pia ni mwanasheria, Osama Alam, ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, angeliendelea kubakia kwenye uwanja huo, hata kama atakufa.

"Sisi waandamanaji ndio jeshi la uwanja huu, na tutakufa hapa. Kama nitakufa hapa, familia yangu itaona fahari, maana nimekufa nikiipigania nchi yangu." Amesema Alam.

Hata hivyo, jeshi, ambacho ni chombo kinachoheshimiwa sana nchini humo, kimeshasema wazi kwamba, kamwe hakitatumia nguvu dhidi ya waandamanaji, madhali tu wanatumia njia za amani kutoa madai yao. Msemaji wa jeshi hilo, Ismail Etman, amesema kwamba jeshi ni mali ya wananchi na lipo kwa ajili yao.

"Jeshi linapata uhalali wake kutoka kwa umma na si kinyume chake. Tunataka kuwathibitishia kuwa jukumu letu sisi ni kulinda usalama wa nchi yetu na mipaka yake na kwamba tunatambua haki ya raia kutoa maoni yao kwa njia za amani, na hatutomshambulia raia yeyote yule." Amesema Etman.

Na licha ya shirika la usafiri wa treni nchini humo kusitisha shughuli zake leo hii, kwa lengo la kuwazuia waandamanaji wasifike kwenye maeneo yaliyopangwa, maandamano kama haya yanaendelea pia katika miji ya Alexandria, Suez na Ismailia.

NGOs zamtaka Mubarak ajiuzulu

Waandamanaji wakiwa kwenye uwan´ja wa TahrirPicha: picture alliance/dpa

Wakati huo huo, taasisi 50 zisizo za kiserikali nchini Misri, zimemtaka Mubarak kuondoka madarakani, ili kuzuia umwagikaji damu unaoendelea, ambapo hadi sasa watu wapatao 125 wameshauawa, tangu maandamano yaanze wiki moja iliyopita.

Hatua alizochukua Mubarak: za kuvunja na kuunda upya baraza lake la mawaziri, kuahidi mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa; pamoja na kumtangaza makamo wa rais, kwa mara ya mwanzo tangu aingie madarakani miongo mitatu iliyopita, hazijatosha kuwanyamazisha waandamanaji.

Kwengineko duniani, mgogoro huu wa Misri unaendelea kutikisa taasisi za kifedha za kimataifa. Leo hii, Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Dominique Strauss-Kahn, amezionya serikali ulimwenguni kupambana vikali na tatizo la ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa katika mapato, au vyenginevyo zitakabiliana na vita.

Akizungumza akiwa nchini Singapore, Bwana Strauss-Kahn, amesema kuwa, japokuwa taasisi yake iko tayari kuisaidia Misri kujijenga upya, baada ya machafuko ambayo yanaendelea kuuchafua uchumi wake, bado ni jukumu la serikali nyengine duniani kujifunza kuwa upandaji wa bei za chakula, unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa jamii za nchi masikini.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW