1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yachacha Libya

21 Februari 2011

Nchini Libya,miji kadhaa ikiwemo Benghazi na Sirte imegubikwa na maandamano ya kumpinga kiongozi wao Muammar Gaddafi.

Waandamanaji mjini BenghaziPicha: dapd

Kulingana na shirika moja la kutetea haki za binadamu IFHR,kiasi ya watu kati ya 300-400 wameuawa katika ghasia hizo.Wakati huohuo,Ujerumani na Uingereza zimeutolea wito Umoja wa Ulaya kuichukulia Libya hatua kali.Libya nayo imetishia kuwa haitoshirikiana na jumuiya hiyo katika suala la kuwadhibiti wahamiaji haramu.Maandamano hayo yameingia siku yake ya saba.

Picha iliyoonyeshwa kwenye mtandao wa Youtube ya maandamano LibyaPicha: picture-alliance/dpa

Ngome ya upinzani

Miji kadhaa ya Libya ikiwemo Benghazi na Sirte imegubikwa na maandamano yanayoupinga uongozi wa Kanali Muammar Gaddafi ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 41.Maandamano hayo yanaripotiwa kuwa makali zaidi katika mji wa Benghazi ulio ngome ya upinzani na pia Sirte anakotokea Kanali Muammar Gaddafi.  

Wakati huohuo,Uingereza na Ujerumani zimeutolea wito Umoja wa Ulaya kuichukulia Libya hatua kali na kusisitiza kuwa jumuiya hiyo kamwe haipaswi kuzikubali kauli za nchi hiyo kuhusu uhamiaji.Ifahamike kuwa Libya imekuwa ikitishia kuwa huenda ikausitisha ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya katika suala la kuwadhibti wahamiaji haramu endapo jumuiya hiyo itawaunga mkono waandamanaji wanaoipinga serikali.

Catherine Ashton:Mkuu wa sera za EUPicha: AP/dapd

EU yawa mkali

Kwa upande wake,Waziri wa masuala ya umoja wa Ulaya wa Ujerumani,Werner Hoyer alisisitiza kuwa hali hiyo kamwe haikubaliki.

Libya ni kituo muhimu kinachotumiwa na wahamiaji haramu kuingia barani Ulaya wakitokea mataifa ya Afrika.Italia inayotatizwa zaidi na wahamiaji hao pindi wanapoingia barani Ulaya,imejitahidi sana kufikia mwafaka na Uongozi wa Libya kuhusu suala hilo.Akizungumza mjini Brussels,Waziri wa Mambo ya nje wa Italia,Franco Frattini aliuelezea umuhimu wa makubaliano hayo.

Waandamanaji wa BenghaziPicha: dapd

Misimamo mikali

Jambo jengine lililojitokeza ni uwezekano wa wanasiasa walio na misimamo mikali ya Kiislamu kuchukua hatamu za uongozi katika nchi hiyo inayopakana na Bara la Ulaya kwa upande wa bahari ya Mediterranea.Kauli nyengine zinaashiria kuwa uwezekano wa kumuwekea vikwazo Muammar Gaddafi nao pia unatathminiwa kama alivyoeleza Waziri wa mambo ya nje wa Finland,Alexander Stubb.Kwa upande mwengine,Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza,William Hague,anaripotiwa kumuamuru balozi wa Libya nchini humo kufika afisini mwake ili kuuelezea msimamo wao unaoyapinga matumizi ya nguvu nyingi dhidi ya waandamanaji.    

Mawaziri hao wa mambo ya nje wanaokutana mjini Brussels wanalijadili suala zito la kuyasaidia mataifa ya eneo la Maghreb ili kuyasaidia kujikita katika mifumo ya kidemokrasia.Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Catherine Ashton anajiandaa kuizuru Misri.

Marekani nayo inasubiriwa kutoa tamko lake kuhusu suala la Libya.Uturuki iliyoiunga mkono Misri,inaifuatilia hali hiyo kwa karibu.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW