Maandamano yaendelea Myanmar
26 Septemba 2007Kulizuka hali ya mvutano katika eneo maarufu la mji mkuu Yangon uliokua ukijulikana zamani kama Rangoon, la Shwedagon Pagoda, baina ya waandamanaji na polisi wa kuzuwia fujo waliofyatua risasi za onyo hewani, kuwa mkon´goto baadhi ya watawa wa kibudha na kuwaingiza wengine kwa nguvu katika malori yaliokua yakisubiri. Utawala wa kijeshi nchini Myanmar iliokua ikitiwa zamani Burma, wamepiga marufuku mikusanyiko yote ya zaidi ya watu watano na amri ya kutotoka nje kuanzia magharibi ahadi alfajiri, baada ya siku nane za maandamano ya kuipinga serikali yakiongozwa na watawa hao katika mji mkuu na miji mengine nchini humo.
Kiasi ya watawa 3,000 na wanafunzi wapatao 4,000 pamoja na wanachama wa chama cha National League for Democracy kinachoongozwa na Bibi Aung San Suu Kyi, walikua wakisubiriwa na polisi wakati wakielekea katika eneo la Sule Pagoda kati kati mwa jiji la Yangon. Bibi Kyi yuko katika kizuizi cha nyumbani. Amekua kiuizini kwa karibu miaka 12 kati ya 18 iliopita.
Kiasi ya watawa 100 walikataa kutii amri ya polisi kuwataka watawanyike. Awali wanajeshi wakiwa na silaha walizifunga barabara zote nne kuu za kuingilia eneo hilo na kuzizingira sehemu muhimu za kukusanyikia waandamanaji hao. Baadhi ya waandamanaji walibeba bendera na jogoo nembo ya chama cha demokrasia .
Katika umoja wa mataifa hotuba za viongozi kadhaa wa nchi za magharibi katika baraza kuu la umoja zimegusia juu ya hali nchini Myanmar huku katika hotuba yake jana (Jumanne) Rais Bush alitangaza hatua kadhaa zaidi dhidi ya watawala wa kijeshi, akisema , “Ninatangaza hatua kadhaa kusaidia kuleta mabadiliko ya amani nchini Burma. Marekani itaimarisha vikwazo vya kiuchumi kwa viongozi wa utawala wa nchi hiyo na wanaowasaidia kifedha. Tutarefusha marufuku ya visa kwa wale wanaohusika na ukiukaji mkubwa kabisa wa haki za binaadamu.”
Kwa upande mwengine Singapore ambayo ni mwenyekiti wa jumuiya ya kimkoa ya kusini mashariki mwa Asia ASEAN leo imewataka watawala nchini Myanmar kuwa na subira na ustahamilivu katika kukabiliana na waandamanaji.Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Singapore ilisema nchi hiyo ina wasiwasi na hali ya mambo nchini Myanmar ambayo pia mwanachama wa jumuiya hiyo ya ASEAN inayoyakusanya mataifa kumi ya eneo hilo.