Maandamano duniani kulaani kuzuiwa misaada kupelekwa Gaza
3 Oktoba 2025
Kuanzia Ulaya, Australia na Amerika ya Kusini, mamia kwa maelfu ya waandamanaji wamejitokeza barabarani kulaani kuzuiwa kwa msafara wa Global Sumud Flotilla, uliokuwa na lengo la kuvunja mzingiro wa jeshi la Israel katika ukanda wa Gaza – eneo ambalo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba linakabiliwa na njaa kali kufuatia karibu miaka miwili ya vita.
Kwa mujibu wa polisi wa Barcelona, takriban waandamanaji 15,000 walijitokeza katika mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Uhispania, wakiimba nyimbo za mshikamano na Wapalestina kama "Gaza, hamuko pekee yenu", "Uhuru kwa Palestina" na "Isusie Israel."
Polisi wa kupambana na ghasia walilazimika kuwatawanya baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuvuka vizuizi, wakitumia virungu na kuwalazimisha kurudi nyuma.
Miongoni mwa meli zilizozuiwa ilikuwa ile iliyombeba aliyekuwa meya wa Barcelona, Ada Colau, pamoja na wanaharakati wengine akiwemo Mandla Mandela, mjukuu wa Nelson Mandela. Ripoti zinaeleza kuwa huenda wakafukuzwa na Israel.
Nchini Ireland, mamia ya waandamanaji walikusanyika mbele ya bunge mjini Dublin, ambapo uungwaji mkono kwa harakati ya Wapalestina hulinganishwa na mapambano ya kihistoria ya Ireland dhidi ya ukoloni wa Uingereza.