1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yageuka mapambano

2 Februari 2011

Kile kilichoanza kama maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Rais Hosni Mubarak kwenye uwanja wa al-Tahrir mjini Cairo, sasa kimegeuka mapambano kati ya waandamanaji na watu wanaotajwa kuwa wafuasi wa Mubarak.

Mapambano kwenye uwanja wa Tahrir
Mapambano kwenye uwanja wa TahrirPicha: AP

Shahidi mmoja ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa mchana wa leo wafuasi wa Rais Mubarak wamewavamia waandamanaji kwenye uwanja wa al-Tahrir na kuwashambuliana kwa silaha za kienyeji, zikiwemo fimbo, mawe na visu.

Kwa uchache, watu kumi wamejeruhiwa hadi sasa, wengi wao wakitoka damu vichwani. Mmoja wa majeruhi hao, Waheed, amesema kuwa alipigwa na wafuasi wa Mubarak.

"Hawa ni majambazi wa chama tawala, NDP. Nilikuwa kwenye mlango wa kuingilia uwanja wa al-Tahrir kuweka uzio wa kibinaadamu, mara kundi likaja na nikasikia jiwe linanipiga kichwani. Lakini ninachotaka Mubarak aondoke tu." Amesema Waheed.

Vikosi vya serikali vyashutumiwa

Mwanajeshi akisoma gazeti juu ya kifaru chake kwenye uwanja wa TahrirPicha: dapd

Mwandamanaji mwengine, Mohammed Zomor, mzee wa miaka 63, ameliambia Shirika la Habari la AFP, kwamba waliowavamia walikuwa ni wafuasi wa NDP na maafisa wa usalama wa taifa, ambao wamevaa kiraia, kwa lengo la kuyachafua maandamano yao ya amani, japokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imekanusha kushiriki askari wake kwenye mapambano haya.

Wakati haya yakitokezea, Al-Jazeera imeripoti kuwa watu waliopanda farasi na ngamia, pamoja na magari ya wafuasi wa Mubarak yanayoendeshwa na watu waliovalia sare za polisi, yalikuwa yakiwasili uwanjani hapo. Kizuizi cha jeshi kilichowekwa, kilishindwa kuwazuia, licha ya kupiga risasi za onyo hewani.

Kuna uwezekano kuwa, jeshi ambalo lilikuwa limejitayarisha kuwalinda tu waandamanaji waliokuwapo mitaani, limejikuta halina uwezo wa kukabiliana na mapambano baina ya waandamanaji na wafuasi wa Mubarak, ambayo yanaonekana ni hujuma iliyopangwa vyema, bila ya uelewa wa jeshi hilo.

Kiongozi wa upinzani, Mohammed El-Baradei, amesema kwamba, kinachotokezea ni dola ya Misri kugeuka na kuwa kundi la wahalifu, ambalo linatumia uhalifu kutisha raia wake, akionya kuwa Misri inaelekea kwenye umwagikaji mkubwa wa damu.

Israel roho juu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amemtaka Rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wengine duniani kutangaza kwamba serikali yoyote mpya itakayoingia madarakani nchini Misri lazima iheshimu mkataba wa amani wa mwaka 1979 kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na mabalozi waliopo Tel Aviv hivi leo, Netanyahu amesema kuwa maslahi pekee ya Israel kwa Misri ni kuona kuwa amani kati yao inadumishwa.

"Israel inaamini kuwa jumuiya ya kimataifa lazima ihakikishe kuwa serikali yoyote ya Misri inaheshimu mkataba wake wa amani na Israel." Amesema Netanyahu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, Israel inataka pawepo orodha ya masharti yatakayowekwa na jumuiya ya kimataifa katika kuitambua serikali yoyote itakayoingia madarakani, ikiwa Mubarak atalazimika kuondoka, kufuatia maandamano yanayoendelea dhidi yake.

Hofu ya Israel, kwa mujibu wa Netanyahu, ni serikali ya Misri kuingia mikononi mwa kundi la Ikhwanul-Muslimin (Udugu wa Kiislamu), ambalo ndilo pekee lililojipanga kisiasa na kimkakati nchini Misri, na hivyo kuja kugeuka Iran nyengine mlangoni pake.

Israel inataka utumike mfano wa pale kundi la Hamas la Palestina liliposhinda uchaguzi wa bunge wa mwaka 2006 na kuwekewa masharti ya kutambuliwa na nchi za Magharibi, yakiwa ni kuitambua haki ya kuwapo taifa la Israel, kukataa matumizi ya nguvu kufikia lengo la Wapalestina kujitawala na kukubaliana na wazo la kuwepo kwa mataifa mawili, la Israel na Palestina.

Hamas iliyakataa masharti yote matatu na hadi sasa imesusiwa na Marekani na nchi za Ulaya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW