1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMsumbiji

Maandamano yaitikisa ngome ya upinzani Msumbiji

Sylvia Mwehozi
17 Oktoba 2024

Vikosi vya usalama nchini Msumbiji vimefyatua risasi kutawanya mamia ya wafuasi wa mgombea wa upinzani Venancio Mondlane, kulingana na video zilizosambaa mitandaoni na Mondlane ambaye anadai kushinda uchaguzi wa rais.

Nampula-Msumbiji-Oktoba 16 2024
Maandamano ya upinzani mjini Nampula MsumbijiPicha: PODEMOS

Vikosi vya usalama nchini Msumbiji jana Jumatano vimefyatua risasi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa mgombea wa upinzani Venancio Mondlane, kulingana na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na Mondlane mwenyewe, ambaye anadai kushinda uchaguzi wa wiki iliyopita.

Mgombea huyo wa upinzani amedai kuwa vijana watatu wamejeruhiwa kwa risasi za moto, na kwamba mmoja wao yuko katika hali mbaya sana kwani alipigwa risasi miguu yote miwili.

Soma: Uchaguzi nchini Msumbiji: Je, upinzani una nafasi?

Idadi ya waliojeruhiwa haikuweza kuthibitishwa kwa uhuru. Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa polisi Gilberto Inguane hakuthibitisha uwepo wa majeruhi yeyote. Inguane amesema polisi walitumia "mbinu za kuwatawanya" baada ya waandamanaji kuwarushia mawe na kuchoma matairi, akiongeza kuwa watu wanne wamekamatwa.

Mgombea urais Venâncio Mondlane baada ya kupiga kura mjini Maputo Picha: Romeu da Silva/DW

Mondlane na mamia ya wafuasi waliandamana katika mji wa kaskazini-mashariki wa Nampula, kupinga tangazo la mamlaka ya uchaguzi lililotolewa Jumatatu kwamba chama tawala cha Frelimo kilishinda uchaguzi wa Oktoba 9 katika jimbo la Nampula kwa asilimia 66.Waangalizi uchaguzi wa Msumbiji watilia shaka mchakato mzima

Jimbo hilo ambalo ni kubwa zaidi nchini Msumbiji, ni ngome ya upinzani. Afisa wa polisi aliuawa katika maandamano huko Nampula mwaka jana baada ya Frelimo kutangazwa kuwa ilishinda uchaguzi wa serikali za mitaa.

Nchi hiyo ilifanya uchaguzi wa rais, bunge na magavana wa majimbo huku chama tawala cha Frelimo kikitarajiwa kushinda. Frelimo imetawala nchi hiyo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno miaka 49 iliyopita. Matokeo rasmi ya nchi nzima yanatarajiwa kutangazwa Oktoba 24.

Mondlane, akiungwa mkono na chama kidogo cha Podemos, alidai ushindi mara tu baada ya siku ya kupiga kura. Ameitisha mgomo wa nchi nzima Oktoba 21 dhidi ya kile anachodai kuwa ni udanganyifu mkubwa.

Mgombea urais wa FRELIMO Daniel Chapo akipiga kura Picha: Mozambique Liberation Front/AFP

Mwanasheria mkuu wa Msumbiji alimuonya Mondlane siku ya Jumanne kwamba kudai ushindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa kunaweza kuchochea machafuko ya kijamii na ni kinyume cha katiba.

Soma pia: Uchaguzi wa rais nchini Msumbiji unakutanisha wagombea wanne

Kulingana na takwimu za Mondlane, alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii, anadai kupata asilimia 53 ya kura katika uchaguzi wa urais kufikia siku ya Jumanne, huku asilimia 67 ya kura zikiwa zimehesabiwa, dhidi ya asilimia 36 za mgombea wa Frelimo Daniel Chapo.