Maandamano yako pale pale Venezuela
11 Mei 2017Wanajeshi wa kikosi cha ulinzi wa taifa walifyatua mabomu ya kutoa machozi, na kundi la wanamgambo wenye silaha wanaoiunga mkono serikali waliwanyanyasa waandamanaji wakati wakijaribu kuandamana kuelekea mahakama kuu.
Mwanamgambo mmoja aliyekuwa amejifunika uso alifyatua risasi kadhaa hewani lakini wanamgambo hao walilazimika kutawanyika baada ya maafisa wa usalama kuingilia kati.
Karibu watu 93 wamejeruhiwa mjini Caracas na muandamanaji mmoja Miguel Castillo ameuawa. Maafisa pia wametangaza kwamba kijana mwingine Anderson Durgarte mwenye miaka 32 ambaye alijeruhiwa kwa risasi siku ya Jumatatu katika maandamano ya mjini Merida naye pia amefariki.
Vurugu hizo zimefanya idadi ya vifo kufikia 38 katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja wa maandamano ya mitaani na msukosuko wa kisiasa. Delsa Solorzano ni mbunge wa upinzani ambaye anamtupia lawama zote waziri wa mambo ya ndani akisema "wewe! waziri Nestor Reverol, ni mtu unayewajibika kwa vifo vinavyotokea Venezuela. Reverol unawajibika kwa yote ninayoyasema!, waziri muuaji kwa sababu muuaji pia anaweza kuwa mtu anayewajibika kimawazo kwa ajili ya vifo sio tu mtu ambaye anaua."
Waandamanaji wanadai kwamba serikali ya kisoshalisti ya Rais Nicolas Maduro imekuwa ya kimabavu na inawajibika kwa mfumuko wa bei ambao umekwenda mara tatu juu, ukosefu mkubwa wa chakula na uhaba wa dawa na kuongezeka kwa uhalifu.
Hata hivyo rais huyo ameziita harakati hizo za upinzani kuwa ni vurugu, na jitihada za mrengo mkali wa kulia zinazolenga kumwondoa madarakani.
Waandamanaji walikuwa wakiandamana kuelekea katikati ya mji wa Caracas huku wakiimba kuwa "sisi ni akina nani? Venezuela! Tunataka nini? Uhuru!". Hata hivyo walifuatwa na wanamgambo waliokuwa wamevalia nguo nyeusi huku wakiwa wamejifunika nyuso zao, karibu watatu kati yao walikuwa wamebeba silaha.
Makamu wa rais wa chama cha kisoshalisti Diosdado Cabello hata hivyo amewalaumu waandamanaji kuwa ndio waliomuua huyo mtu huyo na kwamba mbunge wa upinzani Freddy Guevarra anawajibika kwa ajili ya vifo hivyo na waache kuiitupia lawama serikali.
Zaidi ya watu 1300 wamekamatwa katika vurugu hizo, idadi hiyo haijumuishi raia 250 ambao wameshitakiwa katika mahakama za kijeshi. Maduro ameapa kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo kwa kuitisha bunge maalumu litakalofanyia marekebisho katika ya nchi, ingawa viongozi wa upinzani wamekataa kushiriki.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga