1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yapigwa marufuku Burundi

Mjahida 11 Mei 2015

Serikali ya Burundi imepiga marufuku maandamano zaidi nchini humo ya kupinga uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu, na imewaamuru maafisa katika sekta ya umma kurejea kazini.

Polisi wakijaribu kudhibiti hali mjini Bujumbura Burundi
Polisi wakijaribu kudhibiti hali mjini Bujumbura BurundiPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Marufuku hiyo imetolewa, huku mtu mmoja mwingine akiuawa jana katika mapambano kati ya serikali na waandamanaji wa mjini Bujumbura, wakati wa maandamano ya kumpinga Rais Nkurunziza.

Mtu huyo aliyeuawa kwenye eneo la Musaga, amefikisha idadi jumla ya watu waliouawa nchini Burundi tangu kuzuka kwa maandamano hayo Aprili 25, kuwa 15, huku wengine 216 wakiwa wamejeruhiwa.

Maandamano hayo yalizuka baada ya chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD, kutangaza hatua ya Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi ujao wa Juni. Nadia Muhimpundu ni mmoja wa waandamanaji.

Mmoja wa waandamanaji BurundiPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Aidha, serikali ya Burundi imeamuru maafisa wake wa umma kurejea kazini na shule zote zifunguliwe leo. Tangazo hilo lilitolewa siku ya Jumamosi na Waziri wa Ulinzi, Jenerali Pontien Gaciyubwenge.

Mwanaharakati wa vyama vya kiraia, Pacific Ninihazwe, amesema amri hiyo ya serikali itachochea ghasia zaidi na anashangazwa kuwa waziri wa ulinzi ametoa tangazo hilo, baada ya Mei Pili kusema kuwa jeshi halitoegemea upande wowote na litazingatia mkataba wa Arusha uliofikiwa mwaka 2000, pamoja na kuizingatia katiba ya nchi hiyo.

Waziri Steinmeier wa Ujerumani aizungumzia hali Burundi

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ameelezea wasiwasi wake kutokana na hali inayoendelea nchini Burundi na ametishia ingawa siyo moja kwa moja, kupunguza misaada ya maendeleo kwa nchi hiyo.

Katika barua yake aliyomuandikia waziri mwenzake wa Burundi, Steinmeier ametishia kupunguza misaada ya rasilimali za maendeleo. Ameitaka Burundi kuheshimu demokrasia na utawala wa sheria, pamoja na kuheshimu haki za binaadamu, kwani ndiyo njia itakayosaidia kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande mwingine, Ubelgiji imesema leo kuwa itasitisha msaada wake kwa Burundi katika mchakato mzima wa uchaguzi, kutokana na maandamano ya ghasia kati ya vikosi vya usalama na wanaadamanaji wanaompinga Rais Nkurunziza. Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Ubelgiji, Alexander De Croo, amesema katika taarifa yake kuwa nchi yake pia imesitisha msaada kwa kikosi cha polisi nchini humo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Reuters/S. Loos

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watafanya mkutano wa kilele nchini Tanzania keshokutwa Jumatano, wenye lengo la kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa nchini Burundi, chini ya mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Kikwete amesema wamekubaliana kukutana ili kujadiliana namna ya kuwasaidia ndugu zao wa Burundi, kuweza kufanya uchaguzi wa mafanikio utakaohakikisha taifa hilo linaungana pamoja na kuwa na usalama, bila ya kuwepo mizozo yoyote isiyo na maana.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE,KNA

Mhariri: Iddi Ssessanga