Maandamano yatikisa miji kadhaa ya Marekani kupinga ukatili
31 Mei 2020Kifo cha Mmarekani Mweusi George Floyd katika mji wa Minneapolis wiki iliyopita baada ya kukandamizwa na maafisa wa polisi kimeendelea kuzusha maandamano na vurugu katika miji kadhaa nchini Marekani, na maelfu kwa maelfu ya waandamanaji kujitokeza licha ya amri ya kutotoka nje usiku katika baadhi ya miji.
Katika mji wa Minneapolis, maelfu ya polisi na maafisa wengine wa usalama walishika doria na kuyatawanya maandamano ya vurugu.
Mjini Los Angeles, watu walipora mali kwenye maduka, huku jengo la mahakama mjini Nashville Tenessee likiteketezwa moto.
Waandamanaji pia waliharibu ofisi za polisi katika mji wa Ferguson, Missouri, mji ambao mnamo mwaka 2014, ulikumbwa na maandamano makali mnamo baada ya polisi kumpiga risasi Michael Brown 18, na kumuua.
Mjini Jacksonville jimbo la Florida, afisa mmoja wa polisi alichomwa kisu shingoni, na kulingana na vyombo vya habari nchini humo, afisa huyo anaendelea kutibiwa hospitalini.
Watatu wapiga risasi, mmoja afariki
Kwenye mji wa Indianapolis jimbo la Indiana, watu watatu walipigwa risasi na mmoja kufa.
Katika mji wa New York, video imeonyesha gari la polisi likivurumishwa kwa waandamanaji ambao walianza kulizingira gari hilo na kulishambulia.
Kuhusiana na kisa hicho, meya wa mji huo Bill de Blasio amesema "ni Dhahiri kuwa kuna nia nyingine ambayo imehusishwa kwenye maandamano haya ya watu kujaribu kuwadhuru maafisa wa polisi na pia kuyaharibu magari yao.
De Blasio ameongeza kuwa afisa huyo alikuwa katika hali isiyovumilika na hakuwa na budi kutoroka.
Kwa jumla zaidi ya miji ishirini ilitangaza amri ya kutotoka nje usiku wa kuamkia Jumapili, na hivyo kuathiri mamilioni ya watu mfano Los Angeles, Miami na Chicago huku maafisa wa kulinda usalama wakijaribu kuzuia uharibifu unaoendelea.
Kumbukumbu ya Wamarekani weusi kuuawa kikatili
Kuzidi kwa ghadhabu za watu baada ya kifo cha George Floyd, kumefufua kumbukumbu za namna ambavyo polisi wamewaua baadhi ya Wamarekani weusi nchini humo katika miaka ya nyuma, na sasa maafisa wanatafuta mbinu za kutuliza hasira zao na kusitisha maandamano.
Rais wa Marekani Donald Trump amechukua msimamo mgumu na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya waandamanaji akiwashutumu kwa kuwaita "wahalifu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kushoto”.
Rais Trump amesema mtandao wa Antifa ambao mara nyingi huchochea machafuko kwa njia ya uvunjifu wa sheria, ndio wanahusika kwenye maandamano hayo ambayo yamechochewa na kifo cha Floyd. Trump amesisitiza kuwa utawala wake utayazima maandamano ya vurugu.
Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha Democrat Joe Biden, ameshutumu vurugu, lakini amesema Jumapili kuwa rais wa Marekani wana kila haki ya kuandamana. "Kuandamana kupinga ukatili ni sawa lakini kuteketeza majengo na kufanya uharibifu si sawa” Amesema Biden.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa watu kadhaa walikamatwa katika miji ya Minneapolis, Seattle na New York.
Mnamno siku ya Ijumaa afisa mmoja wa polisi kwa jina Derek Chauvin anayedaiwa kumkandamiza marehemu George Floyd shingoni alikamatwa. Afisa huyo ambaye tayari amefutwa kazi pamoja na wengine watatu ambao hawajakamatwa anakabiliwa na kesi ya mauaji.
Vyanzo: APE, AFPE