1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yazidi kuutikisa mji wa Hong Kong

15 Novemba 2019

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika mitaa ya Hong Kong huku uharibifu mkubwa ukishuhudiwa jimboni humo. Maandamano hayo yanaendelea licha ya onyo la rais wa China Xi Jinping.

Hongkong Protest gegen China & Auslieferungsgesetz
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Ibrahim

Watu wawili akiwemo mzee wa miaka 70 wamefariki dunia wiki hii kufuatia vurugu zilizotokea kati ya waandamanaji na polisi. Polisi imesema imeanzisha uchunguzi dhidi ya kifo cha mzee huyo.

Waziri wa sheria Teresa Cheng jana alianguka mjini London baada ya kuzungukwa na kukabiliwa kwa nguvu na kundi la waandamanaji wanaodai demokrasia. Hata hivyo, hakujeruhiwa katika tukio hilo ingawa polisi ya Uingereza imesema inafanya uchunguzi.

China imelaani tukio hilo pia na imeituhumu Uingereza kwa kuchochea maandamano hayo ya kudai demokrasia Hong Kong.

Maelfu ya wafanyakazi wa serikali pia walijiunga na maandamano hayo huku wakiimba nyimbo za "Simama na Hong Kong" na kuinua mikono yao na kuonyesha ishara ya vidole vitano.

Ishara ya vidole hivyo vitano ni ujumbe wa waandamanaji hao ambao wanataka kupewa haki ya kuchagua viongozi wao pamoja na uwepo wa uchunguzi huru kwa madai ya ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji.

Maandamano yaathiri shughuli

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam Picha: REUTERS

Kila kukicha, hali inazidi kuwa tete Hong Kong. Shughuli za kawaida zikiwemo usafiri na masomo zimeathirika baada ya waandamanaji waliovaa nguo nyeusi kuvamia ofisi za vyuo vikuu na kuharibu treni na kufunga barabara. Kwa mara ya kwanza, vyuo vikuu vimekuwa kama kitovu cha maandamano hayo huku yakienea katika sehemu mbalimbali.

Jimbo la Hong Kong lenye idadi ya watu milioni 7.5 limeshuhudia maandamano tangu mwezi Julai yaliyotokana na hasira dhidi ya utawala wa China unaodaiwa kubana uhuru wa Jimbo hilo. Maandamano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika nyakati za jioni na siku za wikendi yameathiri kwa kiasi fulani uchumi wa Jimbo hilo.

"Unaweza kusema tunafanya uharibifu na kusimamisha shughuli za kawaida katika jamii, lakini hii ndio njia ya kusema Hapana kwa serikali na kuishinikiza serikali isikilize matakwa yetu," alisema Jansen mwenye miaka 33, ambaye ni wakili na mmoja wa waandamanaji.

Licha ya jimbo hilo kuwa chini ya Utawala wa China, Rais wa China Xi Jiping ameonekana kutotoa suluhu la kudumu kuzima maandamano hayo. Mapema wiki hii, waandamanaji walitumia mbinu tofauti iliofahamika kama "Maua kila Mahali" iliolenga kufanya uharibifu mkubwa zaidi jimboni humo, hali ambayo ilionekana kuwashinda nguvu polisi.

Hong Kong ni sehemu ya China chini ya mfumo wa "Taifa moja, mifumo miwili" inayoipatia mamlaka ya juu ya kujitawala.

Chanzo afp, reuters

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW