Maandamano yazidi Myanmar
24 Septemba 2007Kulingana na mshahidi walioko mjini Rangun, mji mkuu wa Myanmar, maandamano ya leo yalikuwa makubwa kutokea tangu mkakati wa kidemokrasi ulipopingwa na jeshi mwaka 1988. Maandamano haya yalianzishwa na watawa wa kibudda wakipinga bei kubwa ya mafuta na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku. Huko Myanmar, watawa wanategemea michango ya wananchi ambao hawana uwezo tena kuwapa watawa vitu vyovyote. Kawaida, maandamano yanazuiliwa mara moja nchini Myanmar na serikali ya kijeshi, lakini watawa hawawezi kupigwa kwa vile wanaheshimika sana katika jamii ya Myanmar. Hata waliruhusiwa kupita mbele ya nyumba ya kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Bi Aung San Suu Kyi, ambaye alishinda katika uchaguzi wa mwaka 1990 lakini hakupata ruhusa ya kutawala. Badala yake aliwekwa katika kifungo cha nyumbani. Leo ni mara yake ya kwanza baada ya miaka kadhaa kuonekana hadharani pale alipofungua mlango wake.
Maandamano haya yanazidi kuwa shinikizo kwa serikali ya kijeshi. Kulingana na balozi wa Uingereza nchini Myanmar, Bw. Mark Canning, ni vigumu kusema hali itaendelea vipi: “Kwa kweli hatujui nini kitatokea sasa. Kutaweza kuwa matokeo mbali mbali. Kwanza maandamano yataweza kupungua, lakini kila siku zikiendelea, uwezekano huu unapungua. Pili, tutaweza kuona njia fulani kwa serikali kuyatuliza1 maandamano, haya lakini mimi ningesema haya yatakuwa maafa makubwa ila tu uwezekano wa kutokea ni mkubwa.”
Hali kwa wananchi ni ngumu sana. Mwezi mmoja uliopita bei ya mafuta iliongezwa kwa mara mbili. Vilevile bei za bidhaa nyingine zimepanda. Hata kabla ya hayo, umaskini umeenea sana. Kila mtoto mmoja kati ya watoto watatu hana chakula cha kutosha.
Alipoeleza juu ya hali nchini Myanmar katika Redio ya Australia, mkuu wa mradi wa vyakula duniani wa Umoja wa Mataifa, Charles Petri, alisema: "Watu wanazidi kuwa na shida kuishi. Tunauona msiba mkubwa wa kiuchumi na kijamii na tunaona kwamba wananchi wanazidi kuwa na dhiki na taabu maishani.”
Jumuiya ya watawa wa dini ya Kibudda iliarifu kuwa maadamano yataendelea kwa amani hadi serikali ya kijeshi itakapoangushwa. Barabarani, watawa waliwaomba wenzao waandamanaji kutotoa miito ya kisiasa bali kuimba sala. Wengi wanahofia ghasia na machafuko kuripuka. Kwa mujibu wa makundi yanayotetea haki za binadamu, waandamanaji 200 walikamatwa.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani alitoa mwito kwa serikali ya kijeshi ya Myanmar kuwaachia huru wafungwa hao pamoja na kiongozi wa upinzani Bi Aung San Suu Kyi. Msemaji huyu alisema pia kuwa serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya zinawaunga mkono waandamanaji. Serikali ya Marekani pia ilitoa mwito kutotumiwa nguvu katika kuyasimamisha maandamano bali kuanza kufanya mazungumzo. Umoja wa Ulaya na Marekani zinataka kuzungumzia suala la Myanmar kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika baadaye wiki hii.
Katika jibu la kwanza rasmi, waziri wa mambo ya dini wa Myanmar, Jenerali Thura Myint Maung, ananukuliwa akisema kuwa serikali itachukua hatua dhidi ya watawa.