1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maas azuru Pakistan

12 Machi 2019

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amekutana na waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan na kujadiliana kuhusu mahusiano baina yao. Khan na Maas pia wamezungumzia hali ya wasiwasi inayozikabili India na Pakistan

Treffen der EU-Außenminister | Bundesaußenminister Heiko Maas
Picha: picture-alliance/dpa/F. Seco

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amekutana na waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan na kujadiliana kuhusu mahusiano baina ya mataifa hayo mawili. Khan na Maas pia wamezungumzia hali ya wasiwasi inayozikabili India na Pakistan pamoja na juhudi za Pakistan za kurejesha amani. 

Mawaziri hao wamejadiliana pia kuhusu usalama wa kikanda pamoja mchakato wa amani nchini Afghanistan.

Mapema hii leo waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi alisema kumekuwepo na hatua zilizofikiwa katika mazungumzo ya amani yanayoendelea Qatar yaliyoingia wiki ya pili sasa na yanayokutanisha wanamgambo wa kundi la Taliban na Marekani. "Inaeleweka kwamba kuna hatua zimepigwa kwa kuangazia mazungumzo ya awali ya amani nchini Afghanistan. Haitarajiwi kuwa rahisi, haijawahi kuwa na wala haitakuwa rahisi." alisema Qureshi.

Alitoa matamshi hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na waziri Maas mjini Islamabad. Hata hivyo hakufafanua zaidi kuhusu hatua hizo, ingawa aliongeza kuwa Pakistan imeendelea kuyahimiza makundi yanayohasimiana nchini humo kukaa pamoja na kuwa na mazungumzo yenye tija baina yao.

Waziri wa mambo ya nje, Heiko Maas akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Imran KhanPicha: Imago/photothek

Maas amewasili nchini Pakistan katika wakati ambapo machafuko katika eneo la Kashmir yakiendelea, lakini pia hali ya kiusalama nchini Afghanistan nayo ikiwa tete. Usalama wa kikanda umekuwa ni ajenda kuu kwenye mkutano na maafisa waandamizi wa Pakistan, ikiwa ni pamoja na waziri mkuu Imran Khan.

Ziara ya Maas nchini Pakistan inakuja wakati jeshi nchini humo likiripoti kwamba watu wawili wameuawa hii leo kwenye mapigano yaliyohusisha vikosi vya Pakistan na India katika eneo linalozozaniwa la Kashmir. Kwenye mazungumzo na waziri Qureshi, amesema Pakistan na India kwa pamoja wana jukumu la kuhakikisha wanazuia machafuko kusambaa zaidi. Aliongeza kuwa mataifa hayo yanahitaji kuhakikisha yanaacha wazi njia za mawasiliano na kuhakikisha wanamaliza mzozo huo.

Akiwa Islamabad, Maas pia anatarajiwa kuzungumzia uungaji mkono wa mashirikiano ya karibu na Afghanistan. Maas, aliwasili katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad akitokea Afghanistan ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi hapo jana. Wakati wa ziara hiyo, aliitaja Pakistan kama "kiungo muhimu kwa Afghanistan imara".

Wakati wa ziara hiyo, Maas pia alitarajiwa kukutana na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Pakistan na kutembelea kituo cha afya cha wakimbizi wa Afghanistan. Amesema Pakistan huenda ikawa ndio yenye jukumu kubwa la kuhakikisha amani nchini Afghanistan.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPE/DW

Mhariri: Sekione Kitojo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW