1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maas yuko Iran kuuokoa mkataba wa nyuklia

10 Juni 2019

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas yuko Iran kuuokoa mkataba wa nyuklia ambao ulifikiwa mwaka wa 2015 ili kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia

Iran Teheran - Heiko MAas und Javad Zarif
Picha: Ilna

. Maas anakutana na mwezake, Mohammad Javad Zarif, pamoja na Rais wa Iran Hassan Rouhani mjini Tehran. Bruce Amani na ripoti kamili))

Akizungumza mapema leo baada ya kuwasili mjini Tehran, Maas amesema kuwa masharti yote ya mfumo rasmi wa malipo kati ya Ulaya na Iran uliobuniwa kuepuka vikwazo vya Marekani sasa yako tayari na utaanza kufanya kazi hivi karibuni. Maas yuko Iran kukutana na Rais Hassan Rouhani na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif, kama sehemu ya juhudi za Ulaya za kuukoa muafaka wa nyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani na pia kuepusha mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran. "Katika mjadala huo, Nchi za Ulaya kila mara zinawakilisha mtazamo wa wazi kabisa. Tunataka kuhifadhi makubaliano haya. Pia tumetambua ukweli kwamba Marekani haijajiondoa tu katika makubaliano hayo, bali pia imetangaza vikwazo upya. Naamini, kuwa Iran lazima pia iwe na nia ya kisiasa katika kuhakikisha kuwa makubaliano haya yanaendelea kuwepo katika siku za usoni".

Rais Rouhani anataka maslahi yake yalindwePicha: Getty Images/AFP

Katika juhudi za kuilinda alau sehemu ya uchumi wa Iran dhidi ya vikwazo vikali vya Marekani na kuuweka hai mkataba wa nyuklia baada ya Marekani kujiondoa, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zimeunda chombo chenye jukumu maalum kinachofahamika kama Instex.

Nchi hizo tatu wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekuwa zikijaribu kuhakikisha kuwa Iran inatimiza ahadi zake chini ya mkataba wa nyuklia za kupunguza shughuli za mpango wake wa nyuklia – ambao Marekani inakosa imani nao – kwa kuisaidia kuepukana na vikwazo vya kibiashara ambavyo Marekani iliiwekea upya.

Zinataka mfumo wa Instex utimize kanuni halali za kutoa fedha zilizowekwa na Jopokazi la maswala ya fedha lenye makao yake mjini Paris, hata ingawa Iran kama nchi haizitekelezi kanuni hizo kikamilifu.

Akiwa Iraq katika safari yake ya kwenda Tehran, Maas alionya kuhusu hatari ambayo mzozo wa Iran inaweka katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati, akisema nchi za Ulaya zinaamini kuwa ni muhimu kujaribu kuudumisha muafaka wa nyuklia na Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran Abbas Mousavi alizikosoa nchi za Ulaya zilizotia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka wa 2015 kwa kushindwa kuuokoa muafaka huo baada ya Rais Donald Trump kuiondoa Marekani mwaka jana na kutangaza upya vikwazo.

Alisema mpaka sasa Iran haijaona hatua zozote za kivitendo na mathubuti kutoka kwa mataifa ya Ulaya ili kuihakikishia Iran maslahi yake. Kwa hiyo Iran haitojadili kingine chochote zaidi ya muafaka wa nyuklia.