1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maaskofu DRC wainyoshea kidole jumuiya ya kimataifa

Jean Noël Ba-Mweze
11 Novemba 2022

Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepaza sauti dhidi ya walichokiita ''unafiki wa jumuiya ya kimataifa'' na kutoa wito kwa Wakongomani kupinga mpango wa kuigawa nchi hiyo.

Kongo Abt Donatien N'shole
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Kauli ya maaskofu wa CENCO imejiri baada ya Mkutano wao maalumu uliofanyika Jumatatu hadi Jumatano wiki hii hapa Kinshasa. Viongozi hao wa kanisa wameituhumu Rwanda kuishambulia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuongeza kuwa mashambulizi hayo ni mpango wa kuigawa Kongo.

Maaskofu hao walizungumzia suala la kudumisha amani katika nchi yao ambako idadi ya watu wanaofariki inaongezeka kila uchao kutokana na vita vinavyoendelea mkoani Kivu Kaskazini. Aidha,  wamelaani walichokitaja kuwa ''unafiki wa jumuiya ya kimataifa'' kama alivyoeleza Askofu Donatien Tshole, Katibu Mkuu wa CENCO.

"Jumuiya hii imetoa vikwazo kwa makundi yenye kumiliki silaha yakiwemo M23. Lakini haikuviwekea Rwanda wakati  inajua vizuri kama waasi hao wanaungwa mkono na Rwanda. Inamaanisha nini kwani jumuiya ya kimataifa ina uwezo wa kusimamisha vita hivi. Kinacholengwa ni nini kama siyo kuigawa nchi yetu. Maaskofu wanakubali mazungumzo, wanakubali diplomasia, lakini eneo la nchi na uhuru wa kitaifa havitajadiliwa."

Maaskofu wa Katoliki wamekuwa na ushawishi katika siasa za CongoPicha: Reuters/T. Mukoya

Raia wa Kongo sasa wana wasiwasi mbele ya Umoja wa Mataifa ambao hadi sasa haujachukua hatua zozote dhidi ya Rwanda na Uganda, nchi zinazotuhumiwa kuhusika katika mzozo wa mashariki mwa  nchi. Lakini ujumbe wa Baraza la Usalama baada ya kuizuru Kongo utakuwa pia katika nchi hizo mbili.  Michel-Xavier Biang, Kiongozi wa ujumbe huo aliomba Wakongo kuuamini Umoja wa Mataifa.Maaskofu wa Congo walaani uhalifu dhidi ya makanisa

"Kongo ni nchi kubwa, Kongo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kongo inaweza kuwa na imani kwa Umoja wa Mataifa kwa sababu umehamasishwa kuunga mkono juhudi za serikali ya Kongo kuleta utulivu mashariki mwa nchi hii. Mipango mingi inayolenga uthabiti wa nchi hii inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa."

Maaskofu hao wa Kanisa wameitisha maandamano ya nchi nzima tarehe 4 Desemba kuimulika hatari inayoikabili nchi yao. Lakini sio wao tu wanaotoa miito ya raia kuingia mitaani, kwani maandamano mengi yanafanyika hapa nchini katika juhudi za raia kuonyesha hasira zao dhidi ya wanachoamini ni mashambulio ya Rwanda na Uganda kupitia waasi wa M23 ambao Kinshasa inawataja kuwa magaidi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW