1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maaskofu wa Congo walaani uhalifu dhidi ya makanisa

Jean-Noel Ba-Mweze2 Agosti 2021

Muungano wa maaskofu wa kanisa katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENCO), umelaani vitendo vya uhalifu linavyotendewa kanisa hilo siku hizi. Vijana wenye hasira walishambulia makanisa na makaazi ya Askofu.

Kongo Abt Donatien N'shole
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Maaskofu walitoa kauli yao baada ya waandamanaji hapo jana kulishambulia kanisa kuu la katoliki mjini Kinshasa pamoja na makao ya Kardinali Fridolin Ambongo, askofu mkuu wa Kinshasa. Baadhi ya wachambuzi wanaeleza kwamba inawezekana mashambulizi haya yemeendeshwa na wafuasi wa chama kilicho madarakani.

Maaskofu wa katoliki wametoa kauli yao leo Jumatatu hapa mjini Kinshasa, wakati wakiwa na sikitiko kuhusu mashambulizi hayo yanayolenga kanisa katoliki.

Waandamanaji walishambulia Jana Jumapili kanisa kuu pamoja na kituo Lindonge ambayo ni makao yake Kardinali Ambongo, Siku chache tu baada ya kanisa la kikatoliki pamoja na lile la kiprotestanti kutomukubali mgombea aliyechaguliwa na makanisa megine ili kuongoza tume huru ya uchaguzi.

Uteuzi wa mwenye kiti mpya wa tume ya uchaguzi

Wafuasi wa chama tawala cha UDPS watuhumiwaPicha: Reuters/K. Katombe

Hayo yamejitokeza wakati hali ni mbaya zaidi huko mkoani Kasaï mashariki, ambako parokia za katoliki zaidi ya kumi zimeshambuliwa na vifaa vitakatifu kuporwa au kuharibiwa. Padri Donatien Tshole ni katibu mkuu wa muungano CENCO.

'' Msahambulizi haya yote yanaonyesha chuki dhidi ya kanisa katoliki.Kadinali Ambongo hakuchukuwa hatua nje ya ile ya kongamano la Maaskofu (CENCO). CENCO inalaani vikali vitendo hivyo vya ugaidi na visivyo kubalika.''  alisema Nshole.

Jambo hili la kanisa kushambuliwa ni jambo haramu, kama anavyoeleza Profesa Nkere Ntanda toka chuo kikuu cha Kinshasa (UNIKIN).

''Ni msangao kuona kwamba magaidi wanashambulia makanisa mchana kutwa na kuvunja vifaa muhimu vya kanisa. Vitendo hivyo haviwafurahishi watu wengi.''

Baadhi ya wachambuzi wanaeleza kwamba mashambulizi haya yanaendeshwa na wafuasi wa UDPS, Chama cha rais Félix Tshisekedi, kutokana na matamshi yenye hasira aliyoyatoa Augustin Kabuya, katibu mkuu wa chama hicho, ingawa yeye mwenyewe anaendelea kukanusha.