1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko ya hali ya hewa, yachangia ukosefu wa maji safi na salama.

Scholastica Mazula15 Mei 2008

Mkutano wa siku mbili kuhusu masuala ya Maji katika nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika -SADC, umefunguliwa jana mjini Maseru, Lesotho.

Raia wa Yangon wakijaza maji kwenye makontena ya maji.Picha: picture-alliance / dpa

Wajumbe wa Mkutano huo wamebainisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yameleta changamoto nyingine katika kuyafikia malengo ya maendeleo ya Milenia yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo ambao umeweza kuwashirikisha wawakilishi kutoka serikalini, makundi ya kiraia, Sekta binafsi, wafadhiri na makundi mengine, umejadili madhara mbalimbali yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika juhudi za kuleta maendeleo kwenye maeneo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Mkutano huo,Mchunguzi na injinia wa masuala ya maji, Torkil Jonch-Clausen, alifafanua kuwa kunahitajika juhudi za vitendo ili kuweza kupata suluhisho la matatizo hayo ili kuzisaidia nchi kuweza kukabiliana na matatizo yaliyopo.

kwa mujibu wa bwana Jonch-Clausen, mabadiliko ya hali ya hewa yameongeza changamoto nyingine katika kuyafikia malengo ya maendeleo ya Milenia.

Malengo nane ya maendeleo ya milenia ambayo yalikubaliwa na viongozi mbalimbali duniani kwenye Mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2000 yalikuwa na lengo la kuongeza kiwango cha maisha ulimwenguni kote hadi ifikapo mwaka 2005.

Lengo la saba ambalo linahusu utunzaji wa mazingira, linazilazimu nchi kutoa idadi ya watu ambao hawapati maji salama.

Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa hivi karibuni katika ripoti ya pamoja baina ya mpango wa usambazaji wa maji na usafi, kwa kushirikiana na Shirika la afya Duniani pamoja na Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, asilimia arobaini ya watu walioko katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara hawapati maji safi na salama.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2004, watu wengi wanaoishi katika maeneo ya vijijini wako hatarini zaidi kuliko wale wanaoishi mijini.

Ni asilimia ishirini na sita tu ya watu walioko vijijini barani Afrika ndiyo wanaopata huduma ya maji safi ikilinganishwa na asilimia hamsini na tano ya wakaazi wa mijini.

Hata hivyo idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi kidogo inatia matumaini, katika nchi za Kusini mwa Afrika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa nchini Botswana imeonyesha kufikia asilimia tisini ya watu wanaopata huduma ya majini.

Nchini Afrika kusini watu asilimia themanini na nane, Zambia na Angola ni asilimi hamsini na nane na asilimia hamsini na tatu inaonyesha nchi ambazo zimepiga hatua fulani katika kuwafikishia maji safi raia wake.

Msumbiji bado ina asilimia ndogo zaidi ya nchi nyingine ikiwa na asilimia arobaini na tatu.Hata hivyo takwimu hizo zinaonyesha mafanikio kutoka asilimia thelathini na sita kwa takwimu zilizotolewa mwaka 1990.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,Juhudi za kutengeneza maji safi na salama katika nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa jangwa la sahara ikiwemo ongezeko la watu, zimekuwa zikitoa kipaumbele kidogo sana katika usambazaji wa maji usafi na salama.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW