Mabadiliko ya hali ya hewa yaonekana barani Afrika
16 Mei 2007Kuona athari za mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika inatosha kuangalia kilele cha mlima wa Kilimandjaro nchini Tanzania na vile barafu inavyopungua. Katika nchi nyingi za Kiafrika wakaazi wanakabiliwa na matokeo ya mabadiliko haya, ikiwa ni pamoja na ukame, mafuriko au mimea kuathiriwa na wadudu waharibifu kutokana na joto kuongezeka.
Nelson Muffah anafanya kazi na shirika la kutoa msaada la Uingereza “Christian Aid”, naye anasikia mara nyingi malalamiko kutoka kwa mashirika mengine nchini Afrika Kusini: “Washirika wetu barani Afrika wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Na pia mafanikio ya juhudi zote za kuleta maendeleo zilizofanywa katika miaka 50 iliyopita yanaangamizwa.”
Mfano mwingine ni Cameroon. Nchi hii ina idadi kubwa ya wanyama na mimea barani Afrika, lakini takriban aina mia moja ya viumbe iko hatarini kuangamizwa. Msitu wa mvua unapungua kutokana na kukatwa miti, kwa sababu watu wengi wanatumia kuni kupika. Nishati inatengenezwa kwa kutumia maji, lakini kutokana na ongezeka la joto na kuenea kwa jangwa, uhaba wa maji unazidi. Anayeangalia kwa karibu mienendo hiyo yote ni Stephan Rostock, ambaye anafanya kazi na shirika la mazingira ambalo linashughulikia kujenga mitambo ya nishati ya maji.
Bw. Rostock anaeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaonekana katika sehemu zote za Cameron, lakini kwa njia tofauti. Na anaongeza: "Kule Kaskazini ambapo ni kavu, ukavu hata unazidi, na Kusini mwenye misitu, jinsi mvua inavyonyesha inabadilika, yaani mvua ikinyesha itakuwa mvua mkali, na kwa hiyo msitu pia unabadilika. Aina ya viumbe vinabadilika. Vile vile pimamaji ya bahari kuzidi kunahatarisha mji wa Duala na viwanda vyake ambao hasa umejengwa juu ya bwawa la matope la pwani. Mji huo italazimishwa kufanyika marekebisha kwa kiasi kikubwa ambacho sisi leo hii hatuwezi kukikadiria.”
Kama anavyoeleza mwenzake Stephan Rostock, Mkamerum Coney Njinkeng, serikali tayari imechukua hatua fulani kupambana na ongezeko la pimamaji. Anaeleza: “Waziri wetu wa mazingira na misitu anajaribu kutafuta mahali ambapo watu wanaoishi kwenye sehemu ziko hatarini kufurikwa watakaoweza kuishi, kama makazi mapya.”
Lakini si wote wakazi ambao wanakubali kuhama. Juu ya hayo isisahauliwe kuwa hatua hizo hazisaidii kutatua chanzo cha mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa hivyo shirika hilo la mazingira linadai hatua zichukuliwe kwenye kiwango cha kimataifa ili kuzisaidia nchi za Kiafrika, mfano kwa kuanzisha mfuko wa kimataifa ambao utakaoweza kuzisaidia nchi maskini kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Fedha pekee lakini hazitatosha, wanasema wanaharakati hao wa Kamerum. Lazima pia kusaidia kitaalamu na kiteknolojia, kuboresha elimu, upatikanaji wa habari na utafiti, ili nchi hizo ziweze kujisaidia na kujiingiza zaidi katika suala hilo la mabadiliko ya hali ya hewa.