1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUlaya

Mabadiliko ya Tabianchi yanavyoathiri wafanyakazi duniani

30 Aprili 2024

Shirika la kazi la umoja wa mataifa ILO, limesema kuwa Idadi kubwa ya wafanyakazi ulimwenguni kote wanakabiliwa na hatari nyingi za kiafya mahali pa kazi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi

Shirika la kazi la umoja wa mataifa ILO, limesema kuwa Idadi kubwa ya wafanyakazi ulimwenguni kote wanakabiliwa na hatari nyingi  za kiafya mahali pa kazi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi, huku likionya kwamba kanuni zilizopo zinatoa ulinzi duni kwa wafanyakazi.

Soma zaidi. Zaidi ya watu 140 wafa kwa radi, dhoruba Pakistan

Katika ripoti yake iloyotolewa Jumatatu wiki hii shirika hilo limesema kuwa Idadi kubwa ya wafanyakazi tayari wanakabiliwa na hatari hizo na huenda idadi hiyo ikaongezeka huku ikibainisha kuwa waathirika wakubwa ni wafanyakazi wa mashambani na wengine wanaofanya kazi nzito katika maeneo yenye hali ya hewa ya joto.

Mwanamke akifanya biashara kwenye jua kali. Picha: Sai Aung Main/AFP

Hatari hizi ni pamoja na joto kupita kiasi, mionzi ya UV ambayo ni mionzi ya jua inayoweza kusababisha madhara kwa ngozi na macho ya binadamu ikiwa inapokelewa kwa wingi bila kinga kama krimu au miwani ya jua, lakini hatari nyingine ni uchafuzi wa hewa,kemikali za kilimo, pamoja magonjwa yanayoenezwa na kusambazwa na viumbe hai kama mbu na nzi ambapo mfano wa magonjwa hayo ni malaria na homa ya dengue. 

Wale wanaofanya kazi katika mazingira yenye joto ndani ya nyumba au nafasi zisizo na hewa ya kutosha pia wako hatarini.

ILO: Asilimia 70 ya wafanyakazi duniani wanafanya kazi kwenye mazingira ya joto

Aidha ripoti hiyo ilibainisha kuwa wafanyakazi ni miongoni mwa watu walio katika hatari zaidi ya mabadiliko ya tabianchi lakini mara nyingi hawana chaguo zaidi ya kuendelea kufanya kazi, hata kama kuna mazingira na  hali ya  hatari.

Manal Azzi, mtaalamu mkuu wa ILO kuhusu usalama na afya kazini, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba mnamo mwaka 2020 mwaka wa mwisho ambao takwimu zinapatikana, wafanyakazi bilioni 2.4, sawa na  zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa ulimwenguni kote, walikadiriwa  kufanya kazi katika mazingira ya joto kupita kiasi kwa wakati fulani, Hii inaashiria ongezeko la wazi la joto duniani. 

Aliongeza kuwa Idadi ya wafanyakazi walioathirika na ongezeko hili imeongezeka  kwa asilimia 35 katika miongo miwili, na kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani,huenda nguvu kazi iliyoathiriwa imeongezeka kwa asilimia 8.8 tangu mwaka 2000.

Kijana akitumia maji kukabiliana na joto kaliPicha: Fabio Teixeira/Anadolu/picture alliance

 Azzi alisema hili ni suala kubwa akionya kwamba  maranyingi wafanyakazi husahaulika dunia inapozungumza juu ya mabadiliko ya tabianchi na athari zake  kiafya ambazo  ni mbaya sana. 

Takriban majeraha ya kazini milioni 23 yanayotokana na joto jingi huripotiwa kila mwaka,huku yakikadiriwa  kugharimu maisha ya watu 19,000 na idadi hiyo haijumuishi zaidi ya watu milioni 26 ambao wanaishi na ugonjwa sugu wa figo unaohusishwa na msongo wa joto mahali pa kazi, ILO ilisema.

Zaidi ya hayo, athari za ongezeko la joto duniani kwa wafanyakazi huenda mbali zaidi ambapo ripoti hiyo ilibainisha kuwa husababisha athari nyingine za kiafya kwa wafanyikazi ikiwa ni  pamoja na saratani, magonjwa ya moyo na mishipa, magonjwa ya kupumua, kuharibika kwa figo na hali ya afya ya akili.

ILO imesema wafanyakazi bilioni 1.6 duniani kote wanakadiriwa kuathiriwa na mionzi ya UV kila mwaka, huku zaidi ya vifo 18,960 vinavyotokana na kazi kila mwaka hutokana na saratani ya ngozi isiyo ya melanoma ambayo husababishwa na mionzi ya UV.

Soma zaidi. Mshirika wa waziri mkuu wa Mali afungwa miaka 2 jela

Hata hivyo kuna uwezekano wa watu wengine bilioni 1.6  kuathiriwa na uchafuzi wa mazingira wa mahali pa kazi, na kusababisha vifo vya hadi wafanyakazi  860,000  walio nje ya mfumo wa kazi.

Mwanaume akiwa na feni kwaajili ya kukabiliana na ongezeko la joto.Picha: Sudipta Das/NurPhoto/IMAGO

Zaidi ya wafanyakazi wa kilimo milioni 870 wana uwezekano wa kuathiriwa na viuatilifu, huku zaidi ya vifo 300,000 vikihusishwa na sumu ya dawa na kemikali za kilimo  kila mwaka pia vifo 15,000 vinavyohusiana na kazi kila mwaka vinahusishwa na mlipuko wa magonjwa yanayoenezwa na vimelea na wadudu, ripoti hiyo ilisema.

Soma zaidi. Mafuriko yasababisha vifo vya zaidi ya watu kumi Nairobi

Manal Azzi, mtaalamu mkuu wa ILO kuhusu usalama na afya kazini alisema ni wazi kuwa mabadiliko ya tabia nchi tayari yanaleta hatari kubwa za kiafya kwa wafanyikazi. hivyo ni muhimu kuzingatia yaliyoainishwa katika ripoti hiyo na mazingatio ya usalama na afya kazini lazima yawe sehemu ya majibu ya mabadiliko ya hali ya hewa sera na vitendo.

ILO ilisema hatari za mabadiliko ya tabia nchi zinaweza kuhitaji nchi kutathmini upya sheria zilizopo au kuunda kanuni mpya za kulinda wafanyakazi ipasavyo. Huku Azzi akiongeza kuwa Shirika hilo litakua mwenyeji  wa mkutano utakaofanyika mwaka ujao wa wataalamu na wawakilishi wa waajiri, wafanyakazi na serikali kujadili suala hilo, kwa lengo la kuja na mapendekezo mapya ya sera.