1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfrika Kusini

Mabaki ya waliopigania uhuru Afrika Kusini yarejeshwa

26 Septemba 2024

Mabaki ya watu 42 waliopigania uhuru wa Afrika Kusini na waliofariki wakiwa uhamishoni katika mataifa ya Zimbabwe na Zambia yamerejeshwa nchini mwao.

Mafuvu ya watu
Mafuvu ya watu Picha: Vacca/Emblema/ROPI/picture alliance

Mabaki hayo yalipokelewa na maafisa wa serikali na wanafamilia katika Kituo cha Jeshi la anga la Waterkloof katika mji mkuu Pretoria baada ya kufukuliwa nchini Zambia na Zimbabwe kwa ajili ya kuzikwa upya katika nchi walikozaliwa.

Hii ilikuwa ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuzisaidia familia kuwa karibu na mabaki ya wapendwa wao waliokufa wakikipambania chama cha African National Congress  ANC  na kile cha Pan Africanist Congress PAC.

Kabla ya utawala wa kibaguzi wa wazungu walio wachache kuhitimishwa mwaka 1994, wanaharakati wengi waliondoka Afrika Kusini wakihofia kukamatwa lakini wengine waliondoka ili kupata mafunzo ya kijeshi katika mataifa mengine, kwa lengo la kurejea nyumbani kufanya mapambano ya kutumia silaha.