Mabenki Uhispania yazidi kuwa na hali mbaya kifedha
8 Juni 2012Wanasiasa barani Ulaya pamoja na wawekezaji duniani kote wanahofu kuwa hali ya kushuka kwa uchumi inayoikabili Uhispania inaweza kuifanya nchi hiyo ishindwe kupata pesa zinazohitajika kuziokoa benki zake bila kuifilisi serikali.
Matarajio kuwa viongozi wa nchi hiyo watalazimika kuomba msaada wa kuinusuru kiuchumi yamezidi kuongezeka.
Taarifa za hivi karibuni kutoka kwa Maafisa wa ngazi za juu kwenye Umoja wa Ulaya, zinasema kuwa Uhispania inatarajia kuomba msaada kutoka katika umoja huo mwishoni mwa wiki hii.
Ombi hilo litafuatiwa na kikao cha mawaziri wa fedha wa Kanda ya Sarafu ya Euro ambapo tamko kuhusu mzozo wa uchumi litatolewa. Hata hivyo serikali ya Uhispania haijasema chochote kuhusiana na taarifa hizo.
Fitch yaishusha Uhispania kwenye kulipa madeni
Wakala wa viwango, Fitch Ratings, imeushusha uwezo wa Uhispania kulipa deni lake la nje kwa alama tatu zaidi. Kiwango cha muda mrefu cha uwezo huo, kimekatwa kutoka alama A hadi B tatu hapo jana, katika wakati ambapo kuna wasiwasi kuwa sekta ya benki ya nchi hiyo iliyo kwenye hali ngumu, huenda ikahitaji msaada wa kifedha kutoka nje.
Awali wakala wa Fitch ulikisia kwamba benki za Uhispania zitahitaji kiasi ya euro bilioni 60 kujiinua upya. Lakini sasa kiwango hicho kimefikia euro bilioni 100, kwa kile ilichokiita "hali ya wasiwasi wa hali ya juu."
Matumaini ya Waziri Mkuu wa Uhispania
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amewapa matumaini wananchi wake na kuwaahidi kuwa atafanya maamuzi sahihi kwa faida ya wote.
"Wengine wanazungumzia Euro bilioni 40 wengine bilioni 80. Yote sawa, juu ya hayo tunaweza kushindana. Lakini mimi ninawajibu wa kutathmini hali ilivyo kwa njia sahihi. Ikiwa nitajua msimamo wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, nitawapa taarifa na nitachukua maamuzi sahihi kwa manufaa ya Wahispania wote" alisema Rajoy.
Mkuu wa kundi la Mawaziri wa Fedha wa Ukanda wa Euro, Jean Claude Junker, alisema hapo jana (Tarehe 7 Juni, 2012) kwamba ukanda huo utasaidia kuzifufua benki za Uhispania, kama ukiombwa. Kiasi cha dola bilioni 126 kinaweza kuhitajika kuziokoa benki za Uhispania kutoka kwenye mzozo wa kifedha unasema wakala wa Fitch.
Kudorora kwa mauzo ya dhamana
Hapo jana nchi hiyo iliuza hati zake za dhamana zenye thamani ya dola bilioni 52, lakini ilibidi iwalipe wawekezaji kiwango kikubwa zaidi cha dhamana kuliko hapo mwanzo.
Mauzo hayo yamefanyika baada ya Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo kwenda mjini Brussels siku ya Jumatano (Tarehe 7 Juni, 2012) kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wenye maamuzi kwenye Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Uhispania sasa wako katika harakati za kutafuta suluhu ya tatizo hilo. Kiwango cha gharama za kukopa cha nchi hiyo kimeongezeka kwa kiasi kikubwa na hivyo kuzilazimisha nchi za Ugiriki, Ureno, na Ireland kutafuta suluhu pia.
Mwandishi: Stumai George/APE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman