Mabingwa wa soka Brazil watakaa mjini Koenigstein wakati wa kombe la dunia
13 Aprili 2006Hoteli watakayoweka kambi mabingwa Brazil wakati wa mashindano hayo ya kombe la dunia ipo kwenye mji uliopo kilomita 20 kutoka mji wa kibiashara wa Ujerumani,Frankfurt.
Wabrazil tayari wamekodisha vyumba vyote 50 vya hoteli ya Kempenski Falkenstein.
Kuanzia mwezi juni kutakuwepo na mabingwa kadhaa wa soka duniani ambao watatua mizigo yao kwenye hoteli hiyo ambako chumba kimoja kinakodiwa kwa gharama kati ya euro 300 na 999 kwa usiku mmoja.
Mkurugenzi wa hoteli hiyo Cyrus Heydarian anasema.
``Wachezaji bila shaka wanataka kukaa mahala karibu na uwanja wa ndege ili waweze kufika haraka mahala kunakochezwa mechi zao.pamoja na hayo lakini wanataka kukaa katika mazingira mazuri ambayo sio mbali na miji mikubwa.Kwa hiyo mji wa Koenigstein ulioko karibu na mji wa Frankfurt ni pahala barabara kabisa kwao’’
Wakaazi wa mji huo unaokaliwa na watu 18 elfu wajawa na furaha ijapokuwa wameanza kuwa na wasiwasi juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa kelele za washabiki wa soka watakaotamani kuwaona wachezaji wao vipenzi.
Karkl-Gustav Schram ambaye ni mmoja wa maafisa wa mji wanahusika na ziara ya Brazil anasema hili ni tukio muhimu zaidi tangu kuzuru eneo hilo,Kaiser Wilhelm 2.
Kaiser Wilhelm 2 mfalme wa mwisho wa Ujerumani alilifungua rasmi jumba la mapumziko ya wanajeshi wa ngazi ya juu katika mji huo mwaka 1909. Takriban karne moja baadae jumba hilo lilibadilishwa na kuwa moja wapo ya hoteli chache barani Ulaya zinazotajwa kuwa hoteli maridadi na ndipo hapo watakapoishi nyota wa soka kama vile Ronaldo,Ronaldinho na Kaka pamoja na wengine katika timu ya Brasil kuanzia Juni 5 hadi 16.
Katika muda huo,Brazil itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Cratia mjini Berlin mnamo juni 13 kisha baadae timu hiyo itahamisha ngome yake hadi mjini Cologne kwa ajili ya mechi zake mbili nyingine ijapokuwa timu hiyo itarudi tena kwenye hoteli yake ya mjini Koenigstein iwapo itafaulu kuingia kwenye robo fainali itakayochezwa mjini Frankfurt hapo juli mosi.
Wafanyikazi wa hoteli hiyo wamekuwa wakifanya maandalizi kwa wiki kadhaa kwa ajili ya wageni hao rasmi.
Wakati huo huo maofisa wa mji huo wametaarisha kiwanja kilichoko kwenye uwanja wa michezo wa mji huo japo kuwa kiwanja hicho ni kidogo sana kwa timu ya Brasil kufanya mazoezi yake
Mazoezi hayo yanatarajiwa kufanyika kwenye uwanja wa mjini Mainz ambao unaweza ukawatosheleza maelfu ya washabiki watakaopendelea kufika kujionea.
Wakaazi wa mji wa Koenigstein itawabidi kuzoea tamasha za mitindo kila aina,pamoja na midundo ya ngoma maarufu ya kibrasil inayojulikana kama samba ambazo zimeandaliwa na maofisa wa mji huo.
Hata hivyo idadi ya wageni watakaomiminika kwenye mji huo haijulikani lakini maelfu ya watalii wakibrasil wameshajiandikisha kwenye hoteli za mjini Kolon lakini baadhi wanatarajiwa kukaa kwenye mji wa Koenigstein kwa japo siku moja au mbili.