1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabingwa watetezi Italia kufahamu hatma yao ya EURO 24

20 Novemba 2023

Kocha wa timu ya taifa ya Ukraine Serhiy Rebrov amesema wachezaji wake wameghadhabishwa kuelekea mechi yao ya kuwania kufuzu mashindano ya Ulaya mwakani dhidi ya Italia, mechi itakayochezwa Jumatatu nchini Ujerumani.

Georgiy Sudakov / Kandanda Ukraine
Mchezaji wa Ukraine Georgiy Sudakov na David Frattesi wa Italia Picha: DeFodi Images/picture alliance

Rebrov amesema ghadhabu za wachezaji wake zimetokana na matamshi ya rais wa Shirikisho la Kandanda Ulaya UEFA Aleksandr Ceferin kwamba iwapo Italia hawatofuzu mashindano hayo ili kulitetea taji lao, basi litakuwa ni "janga."

"Naamini kwamba ni watu wa Ukraine wanastahili kutoa hisia zao kuhusiana na hili. Tunastahili kufikiria mechi yetu. Kama nilivyosema, ni muhimu kwa wachezaji kuwa tayari kwa mechi kisaikolojia. Wanastahili kusahau kila kitu, wasahau kuhusu matamshi yote yaliyotolewa katika vyombo vya habari na kufikiria mechi. Naamini taarifa hizi haziwezi kuwaathiri wachezaji wetu kwa njia yoyote ile, watakuwa na hasira zaidi na kuelewa kwamba ni sisi tu tunaoweza kuleta matokeo mazuri," alisema Rebrov.

Licha ya kushinda mashindano ya Euro ya mwaka 2020, Italia walishindwa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 na sasa wako katika hatari ya kukosa kufuzu kwenye shindano la tatu kuu kati ya 4 jumla.

Italia wana jukumu la kufuzu na kutetea taji lao

Katika kundi lao C, England tayari washafuzu kwa mashindano hayo yatakayokuwa Ujerumani, na sasa Ukraine na Italia ndio wanaowania nafasi ya mwisho katika kundi hilo.

Italia na Ukraine wakipambana katika mechi ya kuwania kufuzu Euro 24Picha: Maurizio Borsari/Aflosport/IMAGO

Lakini kwa upande wake kocha wa Italia Luciano Spalletti anasema, Italia wana jukumu la kufuzu mashindano hayo na kulitetea taji lao walililoshinda huko London mwaka 2021. Kwa sasa timu zote mbili zina pointi 13 katika kundi hilo na vijana hao wa Spalletti, watafuzu iwapo watahakikisha kwamba hawashindwi katika mechi hii ya leo itakayochezwa mjini Leverkusen katika uwanja wa bay Arena.

Lakini hata wakashindwa kuipata nafasi ya pili, Italia wana uhakika wa kucheza mechi ya mchujo ya Nations League kuhakikisha kwamba wanafuzu.

"Hakuna kinachoweza kuwa kizingiti katika azma yetu ya kulitetea taji la Ulaya. Kwa hiyo tuna jukumu la kwenda na kulitetea kwa kuwa wachezaji wengi waliopo hapa wanafahamu jinsi ilivyokuwa kazi ngumu kulite taji hilo nyumbani. Na sasa tutakuwa tayari," alisema Spalletti.

Kufikia sasa ni jumla ya timu 17 zilizofuzu miongoni mwao zikiwa, wenyeji Ujerumani ambao wamefuzu moja kwa moja kama waandalizi, wengine ni Ubelgiji, England, Ufaransa, Ureno, Uhispania, Uholanzi na Denmark miongoni mwa timu nyengine.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW