Mabomu ya machozi yatumika kutawanya waandamanaji Sudan
4 Januari 2022Waandamanaji walikuwa wakipiga kelele za kukataa utawala wa kijeshi, na kutoa madai ya kuvunjwa kwa baraza tawala la Sudan linaloogozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alieongoza mapinduzi ya Oktoba 25 na kuuondoa utawala wa mpito wa kiraia.
Maelfu ya waandamanji wameshuhudiwa kote Sudan, ikiwemo katika mji mkuu Khartoum na mji wake pacha wa Omdurman pamoja na mji wa mashariki wa Port Sudan, kadhalika katika mji wa Darfur Kusini wa Nyala.
Soma pia: Marekani yahimiza utawala wa kiraia baada ya Hamdok kujiuzulu
Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alipinduliwa katika mapinduzi ya Oktoba, lakini alirejeshwa madarakani baada ya mwezi mmoja kufuatia makubaliano na jeshi yaliotafuta kutuliza mzozo na maandamo ya kupinga mapinduzi.
Hamdok aliachia nafasi hiyo siku ya Jumapili kufuatia mkwamo wa kisiasa, akisema alishindwa kupata muafaka kati ya majenerali wanaotawala na vuguvugu la kutetea demokrasia.
Sudan imedhoofika kisiasa tangu mapinduzi ya Oktoba 25, yaliofanyika miaka mwili baada ya uasi wa umma uliolaazimisha kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Omar al-Bashir na serikali yake inayoegemea mrengo wa kidini mwezi Aprili 2019.
Soma pia: 2021: Mwaka mapidunduzi ya kijeshi yaliporejea Afrika
Kwa mujibu wa wanaharakati, serikali imaefunga barabara muhimu na mitaa katika mji mkuu Khartoum pamoja na Omdurman kufuatia vuguvugu la maandamano hayo.
Idadi ya vifo yazidi kupanda
Tangu mapinduzi, karibu waandamanaji 60 wameuawa na mamia wengine kujeruhiwa katika ukandamizaji mkubwa unaotajwa kufanywa na vikosi vya usalama. Hii ni kulingana na kundi la madaktari nchini humo.
Soma pia: Kujiuzulu kwa Hamdok huenda kukarejesha staili ya uongozi wa Bashir
Maandamano ya leo yameitishwa na chama cha wataalamu wa Sudan na Kamati ya Upinzani, makundi ambayo ndiyo yalikuwa vinara wa uasi dhidi ya al-Bashir.
Vuguvugu la maandamano linasisitiza juu ya serikali kamili ya kiraia kuongoza kipindi cha mpito, dai ambalo limekataliwa na majenerali wanaosema watakabidhi madaraka kwa serikali iliyochaguliwa.
Uchaguzi nchini humo umepangwa kufanyika Julai 2023, kufuatana na waraka wa kikatiba unaoongoza kipindi cha mpino.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuwepo na majadiliano ya tija kati ya vyama vyote vya Sudan, ili kufikia suluhu ya kudumu, kulingana na msemaji wake Stephane Dujjaric.
Kulingana na afisa wa kijeshi na kiongozi wa maandamano, ambao hawakutaka kutajwa majina, majadiliano yamekuwa yanafanyika kutafuta mtu asiekuwa na mafungamano ili kuongoza baraza la wataalamu hadi uchaguzi utakapofanyika. Miongoni mwa majina yanayotajwa ni la waziri wa zamani wa fedha Ibrahim Elbaradawi.
Chanzo: Mashirika