'Mabunge ya mitaani' Kongo yajadili mabadiliko ya kisiasa
15 Aprili 2026
Katika mikutano hiyo ya wazi, wananchi huimba kauli mbiu za kumuunga mkono rais, wakisema anaongoza suluhisho la changamoto za taifa. Mijadala hii hupangwa kwa njia isiyo rasmi na hutumika kupima na kusambaza mawazo ya kisiasa kutoka kwa walio madarakani.
Bunge la kusimama yana mizizi yake katika miaka ya 1970, wakati lilipotumiwa kupinga utawala wa kidikteta wa Mobutu Sese Seko, likiongozwa na mwanasiasa wa upinzani wakati huo, Etienne Tshisekedi, baba wa rais wa sasa. Kwa mujibu wa katiba ya sasa, rais anaruhusiwa kuhudumu mihula miwili tu, lakini tangu achaguliwe tena, Tshisekedi ameashiria uwezekano wa kufanya mabadiliko, akisema katiba ina mapungufu na haiendani na hali halisi ya nchi.
Wachambuzi wa siasa wanasema mikutano hii inatumika kuhamasisha uungwaji mkono wa mabadiliko ya katiba, ingawa chama tawala kinadai kuwa hakuna maelekezo rasmi yanayotolewa. Upinzani unaonya kuwa hatua hiyo ni jaribio la "mapinduzi ya kikatiba” na umetishia maandamano iwapo itatekelezwa.
Juhudi za mabadiliko zilisimama kutokana na vita mashariki mwa nchi, hasa baada ya kundi la M23 kudhibiti miji muhimu ya Goma na Bukavu. Hata hivyo, baada ya mapigano kupungua, mjadala huo umeanza kufufuka, huku mitaa ikitumika kama jukwaa la kupima maoni ya wananchi.
Jean-Claude Mwamba, mratibu wa mabunge ya kusimama wa chama tawala cha UDPS, anaamini kuwa mabadiliko ya katiba ni hatua inayofuata baada ya vita kumalizika: Kimsingi, tukimaliza vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hapo ndipo tutabadilisha katiba. Hayo madai ya hatari hayatatokea hapa.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa chama tawala, Leon Niondo, anasema kipaumbele cha sasa si muhula wa tatu kwa Rais Tshisekedi, bali ni kurejesha amani kwanza kabla ya mjadala huo kuendelea. Lakini wengine kama Abel Mutombo, mfanyakazi wa shirika la umma na mshiriki wa mikutano hiyo, mtazamo wao ni kutaka katiba ibadilishwe kabisa. "Katiba ya sasa ni kama mkataba wa kuuza nchi. Tunataka kuirejesha nchi yetu kwa kubadilisha katiba. Hiyo ndiyo sababu kuu."
Mvutano kati ya Rais Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila umejikita katika historia ya katiba ya sasa, ambayo ilipitishwa mwaka 2006 wakati wa utawala wa Kabila. Sasa wawili hao wamekuwa mahasimu wa kisiasa, huku kambi ya Kabila ikipinga vikali juhudi zozote za kubadili katiba, ikisisitiza kulinda ukomo wa mihula ya urais.
Wakati huo huo, Kabila amekuwa akihusishwa na mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo, ambapo serikali ya Tshisekedi na baadhi ya wachambuzi wanadai ana ushawishi wa kisiasa au wa moja kwa moja katika mgogoro huo—madai ambayo yamezidisha mgawanyiko wa kisiasa na kuongeza uzito wa mjadala kuhusu mustakabali wa katiba na uongozi wa nchi.
Mashirika