1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko mapya yaikumba Iraq, Iran yafunga mpaka

30 Agosti 2022

Idadi ya waliouawa nchini Iraq imepindukia 20, huku wanamgambo wa ulamaa wa Kishia mwenye ushawishi mkubwa wakikabiliana na vyombo vya usalama katika eneo mashuhuri la Green Zone na Iran ikifunga mipaka yake.

Irak nach al-Sadr Rücktritt eskaliert die Gewalt
Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Wanamgambo wa Saraya Salam wanaotajwa kuegemea upande wa Muqtadha al-Sadr asubuhi ya Jumanne (30 Agosti) walirusha mabomu kwa kutumia makombora kuelekea eneo la Al-Minṭaqah al-Hadhraa (Ukanda wa Kijani) wakati vyombo vya usalama vya Iraq navyo pia vikijibu kwa mashambulizi.

Jeshi la Iraq lilisema makombora manne yalirushwa kuelekea eneo hilo ambalo lina ulinzi mkali.

Picha za moja kwa moja za televisheni zilionesha ghasia hizo, huku mtu mmoja akijeruhiwa karibu sana na jengo wizara ya mambo ya kigeni ya Iraq.

Idadi ya waliouawa tangu machafuko yalipoanza siku ya Jumatatu (29 Agosti) ilikuwa imefikia 22 asubuhi ya Jumanne, kwa mujibu wa maafisa wawili wa afya walionukuliwa na shirika la habari la Associated Press. 

Wanamgambo wa Saraya Salam waliamua kukabiliana na vikosi vya usalama vya Iraq kulipiza kisasi mauaji ya wafuasi wa al-Sadr wasiokuwa na silaha.

Kwa mujibu wa maafisa wawili wa vyombo vya usalama waliozungumza na shirika la habari la Reuters, wanamgambo hao pia walitwaa udhibiti wa makao makuu ya kundi jengine la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika miji ya kusini mwa Iraq usiku wa kuamkia Jumanne.

Iran yafunga mipaka

Moshi ukionekana kwenye eneo la Al-Mintaqah Al-Hadhraa mjini Baghdad asubuhi ya Jumanne (30 Agosti 2022)Picha: Sabah Arar/AFP

Iran, ambayo inashutumiwa na upande wa Al-Sadr kwa kujihusisha na siasa za ndani za Iraq, ilitangaza kufunga mpaka wake kwa kile ilichosema ni "machafuko" na "amri ya kutotoka nje" iliyotangazwa katika baadhi ya maeneo nchini Iraq.

Televisheni ya serikali ya Iran iliwataka raia wa nchi hiyo kuepuka safari za kwenda Iraq na kwa mahujaji wake waliokuwa tayari ndani ya Iraq kutokwenda kwenye miji mingine kando na waliyopo sasa.

Mamilioni ya Wairani huzuru mji wa Kerbala nchini Iraq kila mwaka kushiriki kile kiitwacho "Arubaini", maadhimisho ya siku 40 za kuomboleza mauaji ya Hussein, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W). Mara hii Arubaini hiyo inaangukia tarehe 16 na 17 Septemba. 

Mkwamo wa kisiasa

Ulamaa wa Kishia mwenye ushawishi mkubwa nchini Iraq, Muqtadha Al-Sadr.Picha: Alaa Al-Marjani/REUTERS

Serikali ya Iraq ipo kwenye mkwamo wa kisiasa tangu chama cha Al-Sadr kushinda wingi wa viti kwenye uchaguzi wa bunge wa mwezi Otoba, lakini kushindwa kupata viti vya kutosha kuunda serikali peke yake.

Hadi anaamuwa kujiondowa kwenye majukumu yote ya kisiasa mapema wiki hii, ulamaa huyo alikuwa amekataa kabisa kusaka muafaka na mahasimu wake wanaoungwa mkono na Iran na alijitowa kwenye mazungumzo ya kuutatuwa mkwamo huo. 

Hatua ya hivi karibuni ya kujiuzulu ghafla imeugeuza mkwamo huo wa kisiasa kuwa machafuko, huku pakiwa hapajulikani hatima yake.

Ulamaa huyo anajipatia nguvu kubwa kutokana na uwezo wake wa kuhamasisha umma na kudhibiti sehemu kubwa ya wafuasi wake walio kwenye ngazi za mashinani, lakini tamko lake la kuachana na siasa liliashiria kuwapa wafuasi wake uhuru wa kujiamulia na kujitendea watakavyo. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW