Machafuko mengine yaripotiwa nchini Sudan
2 Agosti 2005
Mashahidi katika kijiji cha Shantytown, umbali wa kilomita 10 tu upande wa kusini kutoka mji mkuu Khartoum, wamesema kuwa wakaazi wenye asili ya kusini, wamewashambulia wale wenye asili ya kiarabu ambao ni kutoka kaskazini.
Habari hizo za ghasia zimethibitishwa pia na waandishi wa habari walioko huko.
Ripoti zimesema kuwa polisi kadhaa wa kutuliza ghasia wametumwa katika kijiji chenye machafuko cha Shantytown huku ndege za kijeshi za helikopta, zikionekana zikizunguka juu ya anga la kijiji hicho.
Hadi hivi sasa, haijafahamika hasara imeshatokea kufuatia machafuko hayo, yanayoendelea kwa siku ya pili mfululizo tangu kifo cha John Garang kilipotangazwa rasmi.
Kwenye mji mkuu Khartoum, hali ni shwari kiasi. Lakini ghasia za jana zilisababisha hasara kubwa. Taarifa za karibuni kabisa zinasema kuwa watu 36 waliuawa. Duru za kidiplomasia zinazungumzia watu 42 waliyouawa na wengine kiasi ya 100 waliyojeruhiwa na ambao sasa wamelazwa katika hospitali.
Maduka na magari kadhaa viliharibiwa vibaya.
Mkaazi mmoja ambae anamiliki duka la simu za mikononi kati kati mwa mji mkuu Khartoum, amesema kuwa “walikuja, akimaanisha wafuasi wa Garang, na kuyachoma moto maduka yote yaliyoko katika sehemu hii. Tulipoteza mali nyingi”, amemalizia kusema Mohammed Hassan, ambae ameshangaa kuona kuwa leo hali ya utulivu imerejea barabarani.
Serikali imeimarisha ulinzi katika mji huo na kutangaza hali ya kefyu kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 alfajiri.
Polisi wa kuzima fujo wameshika doria katika vituo muhimu kama daraja na sehemu ambazo zilizoathiriwa na waandamanaji wa jana.
Yameonekana pia makundi ya kiraia ya kujihami ambayo yameundwa na watu kati ya 10 na 15.
Marekani ambayo kwa muda wote ilikiunga mkono chama cha SPLM cha marehemu John Garang, imewatuma wajumbe wake wawili katika sehemu ya kusini, kudhaminia umoja kwenye uongozi wa chama ambao umekabidhiwa Salva Kiir Mayardit. Serikali ya Sudan imeutuma pia ujumbe wake katika mji wa Rumbek, makao makuu ya zamani ya Garang ambako maiti imefikishwa.
Wapiganaji wa zamani, mashabiki na familia ya John Garang, wamekusanyika mjini humo kutoa heshima zao za mwisho.
Chama cha SPLM kimetangaza msiba wa siku tano katika eneo zima la kusini kuomboleza kifo cha kiongozi wake na kwamba mwili wake utasafirishwa hadi mji mkuu wa eneo la kusini wa Juba kwa mazishi.
Wakaazi wa mji mkuu Khartoum hawatomuona jicho la mwisho John Garang kuepusha machafuko zaidi, kimesema chama cha SPLM.
Chama hicho kinatarajia sasa kuwa kiongozi wake mpya Bwana Salva Kiir Mayardit, atakabidhiwa wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais, aliyekuwa amechukua rasmi Garang waki tatu tu zilizopita. Hayo ni katika kutekeleza mkataba wa amani ambao ulitiwa saini mnamo mwezi Januari mwaka huu.
Ingawaje serikali na viongozi wa chama cha SPLM wanatuliza nyoyo kwamba mpango wa amani utatekelezwa kama ilivyopangwa, wakaazi wengi wa kusini wanahisi kuwa wamepoteza dhamana ya mpango huo.