1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko Tunisia yatikisa nchi za Kiarabu

11 Januari 2011

Vyombo vya habari vya nchi za magharibi vyaonekana kutoyapa kipaumbele maandamano ya Tunisia. Polisi imetumia nguvu kupita kiasi kuyavunja maandamano hayo ya kuipinga serikali ya rais Ben Ali.

Waandamanaji wakimtaka rais Ben Ali, ajiuzluPicha: AP

Maandamano nchini Tunisia ya kuipinga serikali ya rais wa nchi hiyo, Zine el Abidine Ben Ali, yameutikisa ulimwengu wa mataifa ya kiarabu. Hata hivyo vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi vinaonekana kutoyapa kipaumbele maandamano hayo yaliyogubikwa na machafuko, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 14. Sekione Kitojo anaangalia matukio hayo katika nchi hiyo inayoonekana na mataifa ya magharibi kuwa mfano bora.

Ajira na uhuru wa kujielza ni kiini cha maandamanoPicha: dapd

Wakati vyombo vya habari na viongozi wa nchi wakionyesha malalamiko yao nchini Marekani na barani Ulaya wakati wa maandamano kama hayo dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Iran katika mwaka 2009, matukio hayo nchini Tunisia ambayo hayakutarajiwa yalipuuziwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi. Waandishi wa blog katika mtandao wa intaneti pamoja na tovuti ya twita hivi sasa ndio vyanzo muhimu kwa ajili ya kupata taarifa za maendeleo ya kila siku katika machafuko hayo.

Maandamano yatazamwa kupitia mtandao

Waarabu katika mataifa ya mashariki ya kati wamekuwa wakiangalia kwa mshangao kupitia video za mtandaoni pamoja na matangazo ya kituo cha televisheni cha Al-Jazeera yakiwaonyesha Watunisia , ambao wanaonekana kuwa ni watulivu sana , wakifanya maandamano mitaani pamoja na migomo ya kukaa chini dhidi ya polisi wa serikali ya rais Ben Ali.

Utawala wa Ben Ali unatoa picha ya utawala wenye msimamo wa kati unaoungwa mkono na mataifa ya magharibi ambao unaudhibiti mkali dhidi ya umma wa nchi hiyo wakati utawala huo ukifuata msimamo wa mataifa ya magharibi katika mashariki ya kati.

Vijana wanadai ajira mpya watakapomaliza masomoPicha: picture-alliance/dpa

Cheche za hali hiyo ya ghasia , ambapo hivi sasa imedumu kwa zaidi ya wiki tatu, zimetokana na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26, mwenye shahada ya chuo kikuu na ambaye hana kazi, Mohammed Buazizi, ambaye amejichoma moto katika mji wa kati wa Sidi Buzeid akipinga kukamatwa kwa mkokoteni wake wa matunda na mboga.

Jaribio la Buazizi la kujiua lilifuatiliwa na jaribio jingine kama hilo lililofanywa na karibu vijana wawili ambao wamemaliza elimu ya chuo kikuu wakipinga dhidi ya ya hali mbaya ya kiuchumi katika taifa hilo.

Kama ilivyo kwa machafuko yanayotokea katika nchi kadha za Kiarabu zinazoungwa mkono na mataifa ya magharibi, polisi walijibu ghasia hizo kwa matumizi makubwa ya nguvu. Kuna ripoti za matumizi ya risasi za moto, msako wa nyumba kwa nyumba kuwakamata wanaharakati, watu kadha kutiwa mbaroni pamoja na mateso dhidi ya watu waliokamatwa.

Polisi yatumia nguvu kupita kiasi

Polisi kimsingi walivunja maandamano katika mji wa Sidi Buzeid baada ya kukata mawasiliano yote pamoja na barabara katika mji huo, lakini walikabiliana na maandamano zaidi katika miji kadha ya jirani.

Matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji MisriPicha: AP

Misri ilitumia mbinu hizo hizo dhidi ya ghasia zilizofanywa na wafanyakazi wa viwandani katika mji wa viwanda wa Al-Mahal el Kobra hapo April 16, mwaka 2007, na kuzima ghasia hizo katika muda wa siku nne tu baada ya utawala wa nchi hiyo kufanikiwa kudhibiti ripoti za vyombo vya habari ndani ya mji huo, na vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa ama vilipuuzia matukio hayo ama vilichukulia kuwa matukio madogo tu.

Lakini tofauti na ghasia za Misri, kuna ripoti za maandamano na mapambano ambayo yamesambaa nchini Tunisia hadi katika miji ya Gandouba, Qabes na Genyana.

Utawala wa Ben Ali unashutumu, watu wenye msimamo mkali, na wanaochochea ghasia, pamoja na kundi dogo la mamluki, kwamba ndio wanaochochea ghasia hizo, ikiwa ni shutuma maalum ambazo hutolewa na watalawa wa Kiarabu kila kunapokuwa na ishara za hali isiyo ya utulivu miongoni mwa wananchi wao wanaokandamizwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo/IPS
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi