Ukosefu wa mafuta wazusha machafuko ya kimadhehebu lebanon
30 Agosti 2021Mvutano kuhusu ukosefu wa mafuta nchini Lebanon umechochea mgogoro wa kimadhehebu kati ya waislamu wa madhehebu ya Shia na wakristo kusini mwa nchi hiyo.
Mvutano uliosababishwa na hali ya ukosefu wa mafuta ulizuka kwenye vijiji jirani Kusini Mwa Lebanon kati ya waislamu wa madhebu ya Shia na wakristo na duru za usalama zinasema, jeshi lililazimika kuingilia kati.
Mivutano inayosababishwa na suala hili la ukosefu wa mafuta ya petroli na diesel imekuwa ni jambo linaloshuhudiwa kila siku nchini humo hali inayoongeza wasiwasi kuhusu nchi hiyo kutumbukia kwenye machafuko baada ya miaka miwili ya kuwa kwenye mporomoko wa kiuchumi uliotokana na kuanguka kwa mabenki.
Kiasi watu 6 walijeruhiwa katika mvutano wa mwishoni mwa juma uliowahusisha wakristo katika kijiji cha Maghdouche na waislamu washia wa kijiji jirani cha Ankoun.
Inaarifiwa kwamba hii leo Jumatatu hali imerudi kwenye utulivu.Tukio hilo lilichochewa na hatua ya mkaazi wa kijiji cha Maghdouche kupeleka malalamiko polisi baada ya kujeruhiwa wakati wa mvutano kuhusu mafuta mnamo siku ya ijumaa na polisi walikwenda katika kijiji cha Ankoun kuchunguza, lakini wanakijiji walifunga barabara na kuchoma miti na ndipo wanajeshi walipopelekwa katika eneo hilo kwa mujibu chanzo cha habari.
Vurugu hizo zililaaniwa na kiongozi wa chama cha vuguvugu la madhehebu ya Shia la Amal,ambaye ni spika wa bunge la nchi hiyo Nabih Berri, akisema vuguvugu hilo halina mafungamano yoyote, kwa namna yoyote na kilichotokea Maghdouche,akikanusha shutuma zinazotolewa mitandaoni zikilihusisha vuguvugu la Amal. Kuporomoka kwa mabenki nchini humo kumesababisha sarafu ya nchi kushuka thamani kwa zaidi ya asilimia 90 katika kipindi cha miaka 2 na zaidi ya watu nusu milioni wameingia kwenye umasikini. Na hali hiyo hivi sasa imeingia kwenye awamu mpya mwezi huu kutokana na ukosefu wa mafuta jambo lililoifanya sehemu kubwa ya Lebanon kuingia kwenye mkwamo.
Ni hali hiyo iliyomfanya kiongozi wa juu kabisa wa madhehebu ya waislamu wa Sunni Sheikh Abdul Latif Derian kusema ijumaa kwamba nchi hiyo ineelekea kuporomoka kabisa,ikiwa hatua za haraka hazitochukuliwa kumaliza mgogoro uliopo.
Mporomoko wa masoko ya fedha na mabenki nchini humo umetokana na mkwamo wa kisiasa katika nchi hiyo ambayo haina serikali tangu ilipojiuzulu serikali iliyokuwepo mnamo mwaka jana kufuatia mripuko wa bomu katika bandari ya Beirut.
Hivi sasa waziri mkuu mteule Najib Mikati ambaye ni watatu kuchaguliwa kujaribu kuunda serikali mpya,wiki iliyopita alisema kwamba kuna vizingiti vikubwa katika hatua ya kuukamilisha mchakato huo.