1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Machafuko yatishia kuibuka upya Ebola, Beni.

26 Novemba 2019

Shirika la afya ulimwenguni , WHO limesema watoa huduma za kupambana na Ebola bado wamekwama katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia machafuko.

Demokratische Republik Kongo | Überfall auf UN-Lager in Beni
Picha: picture-alliance/dpa/0AP Photo/A.-H. K. Maliro

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Gebreyesus ameandika kwenye ukurasa wa twitter hii leo kwamba kila siku moja ambayo wafanyakazi hushindwa kutoa huduma kikamilifu kwenye maeneo yaliyoathirika huwa ni "janga" ambalo huweza kusababisha kuibuka kwa janga jingine kubwa zaidi la Ebola katika historia ya maradhi hayo.

03.11.2019 Matangazo ya jioni

This browser does not support the audio element.

Wakaazi wa Beni wameghadhabishwa na mashambulizi mabaya yanayoendelea ya waasi licha ya uwepo wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MONUSCO pamoja na vikosi vya serikali ya Congo. Baadhi yao wanashinikiza wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ama kuondoka.

Baada ya mkutano wa dharura hapo jana rais wa Congo Felix Tshisekedi aliamua kuruhusu operesheni ya pamoja ya majeshi ya Congo na Umoja wa Mataifa huko mjini Beni kufuatia maandamano ambayo pia yalisababishwa kuchomwa kwa jengo lililokuwa na ofisi za mji.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanashutumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua za ulinzi wa raia huko Beni.Picha: Reuters/File Photo/O. Oleksandr

Mapema mwezi huu, jeshi la Congo lilitangaza mashambulizi mapya dhidi ya wanamgambo wa Allied Democratic Forces, ADFwaliowaua mamia ya raia pamoja na wanajeshi wa vikosi vya usalama katika kipindi cha miaka michache iliyopita katika eneo hilo la kaskazinimashariki lenye utajiri mkubwa wa madini.

Baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika siku za hivi karibuni kushutumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua ulisema hauna uwezo wa kufanya operesheni katika eneo ambalo tayari vikosi vya usalama vinaendeleza shughuli zake na kwa maana hiyo haviwezi kushiriki kwenye operesheni hizo za kijeshi bila ya kukaribishwa.

Machafuko yoyote kwenye eneo hilo ambako makundi kadha wa kadha ya waasi yanaendeleza shughuli zake yanazorotesha pakubwa juhudi za kupambana na mripuko wa Ebola. Idadi ya visa viliyoripotiwa imepungua na hakuna kisa chochote kilichoripotiwa katika miezi ya hivi karibuni.

Hakuna visa vipya vilivyoripotiwa hivi karibuni, lakini machafuko huenda yakasababisha janga jipya la Ebola.Picha: picture-alliance/dpa/J. Delay

Rais wa Congo aliyeeleza kuumizwa na hali hiyo, amesema mapema mwezi huu kwamba anatarajia mripuko huo unaweza ukamalizika kabisa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo WHO imesema ni lazima zipite siku 42 bila ya visa vipya vya Ebola ili kuthibitisha kwamba mripuko huo hatimaye umeisha.

Zaidi ya visa 3,100 vya Ebola vimethibitishwa tangu ulipotangazwa kuanza mwezi Agosti mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na zaidi ya vifo 2,100. WHO imesema kushuka kwa idadi ya visa vya Ebola ni dalili njema lakini ikionya kwamba maandamano ya hivi karibuni mjini Beni na kwenye maeneo jirani yanatia wasiwasi mkubwa.

Waasi wa ADF wapatao 160 hufanya mashambulizi ya mara kwa mara kote mjini Beni na wamekuwa wakishutumiwa kwa mauaji ya maelfu ya raia pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kurejeshwa utulivu huku akielezea wasiwasi juu ya kusambazwa kwa taarifa za uongo zilizosababisha machafuko yanayoshuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii. 

Mji wa Beni una walinda amani 557 wa Umoja wa Mataifa kutoka Malawi pamoja na takriban maafisa wa polisi 150 kutoka India na walinda amani wengine 150 kutoka Tanzania walioweka kambi kwenye uwanja wa ndege.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW