Machar aonya Sudan Kusini kurejea katika machafuko
21 Oktoba 2019Machar ametaka kucheleweshwa kwa mwezi zaidi ili kutimiza mahitaji ya hatua muhimu katika makubaliano tete ya amani ya taifa hilo.
Machar alitoa ombi hilo kwa ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao ulikutana nae pamoja na RaisSalva Kiir, ukiwa na lengo la kuhimiza kasi ya kupigwa hatua, shabaha ikiwa pia ni kuiondosha Sudan Kusini, kwenye hofu ya vita vilivyodumu kwa miaka mitano ambavyo vimesababisha vifo vya takribani watu 400,000.
Muda wa kuunda serikali ya uliosalia hautoshi
Kiongozi huyo ambae amewasili Jumamosi iliyopita mjini Juba alihoji, kinachoweza kutokea kama ikiundwa serikali hapo Novemba 12 na kuongeza kwamba makubaliano ya kuweka chini silaha kwa pande hasimu ambayo yamedumu kwa takribani mwaka mmoja yanaweza kusamabaratika. "Tunataka kulifanya hili, tunataka kulifanya ili kwa usahihi. Kwa hivyo kama hatutakuwepo tarehe 12, kama Rais Salva, alivyotishia, ataunda serikali tarehe 12, nimewataka wenzangu hapa wasitulaumu. Tuna hali tete, ambayo hatuwezi kuidhibiti. Tunataka hii nchi iwe na amani" alisema Machar."
Lakini balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Kelly Craft alionekana kuvinjwa moyo na onyo la Machar, zaidi alisema "Baraza la usalama limezitolea wito pande zote katika makubaliano kuharakisha mchakato wa kutekeleza mpangilio wa mpito wa usalama, kuendelea na mashauriano ya masuala kadhaa na mipaka ya majimbo na hatiame kuunda kwa amani serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ifikapo Novemba 12".
Marekani kutathimini uhusiano wake na Sudan Kusini
Awali Marekani ilisema kama itatathimi upya uhusiano wake na Sudan Kusini endapo serikali hiyo ya umoja wa kitaifa haijaundwa na kabla ya ujio huu wa Machar nchini humo, ujumbe wa upinzani ulitoa angalizo lililosema pengine kiongozi huyo wa upinzani asingeweza kuwasili nchini humo hadi kuwepo kwa mipango madhubuti ya kiusalama.
Duru za mjadala huu wa sasa zinaonesha inaweza kuchukua angalau miezi mitatu, kutoa mafunzo kwa wapiganaji 41,500 na askari ili kuwafanya kuwa jeshi la pamoja lenye kujumuisha askari wengine 3000 wa ulinzi wa vuiongozi. Serikali ya Sudan Kusini umehitaka jumuiya ya kimataifa kuisadia katika kufanikisha mchakato huo.
Makubaliano ya kwanza ya kuunda serikali ya mgawanyo wa madaraka yalimalizika kwa kuzuka upywa mapigano 2016 na ilielezwa Machar alitoroka taifa hilo kwa miguu. Masuala ambayo yalikuwa yanajadiliwa kwa sasa, ndio yale yale yalisababisha kushindwa kwa mazungumzo yalioshindikana.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Zainab Aziz