1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macho na masikio yaelekezwa Urusi

14 Juni 2018

Tunaanza na homa ya Kombe la kandanda la dunia inayofunguliwa leo mjini Moscow nchini Urusi, ikiwa ni  baada ya miaka kadhaa ya maandalizi ambayo hata hivyo yaligubikwa na mivutano ya kidiplomasia.

Russland Iran Fans in Moskau
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Tunaanza na homa ya Kombe la kandanda la dunia inayofunguliwa leo mjini Moscow nchini Urusi, ikiwa ni  baada ya miaka kadhaa ya maandalizi ambayo hata hivyo yaligubikwa na mivutano ya kidiplomasia. Lakini baada ya yote hayo, hatimaye kipute hicho kitaanza kutimua vumbi viwanjani. 

Wenyeji Urusi, ndio waatakaofungua dimba  dhidi ya Saudi Arabia, katika uwanja wa Luzhniki wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 80,000 ulioko Moscow, baada ya shamrashamra za ufunguzi zitakazohudhuriwa na rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Brazil ina rekodi ya kushinda kombe la michuano hiyo mara tano, huku mabingwa watetezi Ujerumani wenyewe wakishinda mara nne lakini wakipigiwa upatu wa kufikia rekodi hiyo ya Brazil kwenye fainali ya michuano hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wa Luzhniki ifikapo Julai 15.​​​​

Mashabiki wamekwishafika nchini Urusi kushuhudia tamasha hilo kubwa la kombe la dunia.Picha: picture-alliance/dpa/P. Powell

Ulinzi umeimarishwa hususan kwenye eneo la uwanja wa Luzhniki. Polisi wameonakana kurandaranda kuzunguka uwanja huo na hata kwenye maeneo yaliyoko karibu na kituo cha treni. Urusi pia imemwaga maelfu ya polisi katika miji 11 ambayo itakuwa mwenyeji wa mechi nyingine, ili kukabiliana na idadi kubwa ya mashabiki, na hasa mashabiki wakorofi, pamoja na vitisho vingine vya kiusalama.

Baadhi ya mashabiki ambao tayari wako nchini Urusi wameanza kukusanyika na wanaonekana kuwa na furaha kubwa, tayari kushuhudia mechi ya ufunguzi kati ya Urusi na Saudi Arabia.

Waandaaji wa nchini Urusi wanasema wanatarajia zaidi ya wakuu wa nchi 20 kushuhudia mechi ya ufunguzi. Rais wa Urusi Vladimir Putin alinukuliwa alozungumza kwenye mkutano wa shirikisho la soka duniani, FIFA hapo jana akiisifu FIFA kwa kuweka pembeni siasa katika uendeshaji wake kwenye shughuli za soka. Alisema Urusi wakati wote imekuwa ikizingatia misingi ya shirikisho hilo.  

Urusi imetumia zaidi ya Dola bilioni 13 katika kuandaa tukio hili muhimu zaidi tangu ilipoandaa michezo ya Olimpiki ya majira ya joto ya mwaka 1980, mjini Moscow.

Mshambualiaji wa zamani wa Sweden, Zlatan Ibrahimovich ameielekeza karata yake Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden Zlatan Ibrahimovich amesema karata yake anaipeleka kwa timu ya taifa ya Ujerumani, ambayo anaamini itafanya makubwa kwenye michuano hiyo, zaidi ya Brazil na hata Sweden yenyewe, kwa kuwa timu hiyo huwa na wachezaji nyota, si tu kwa wale walio ndani ya uwanja, bali hata walio nje ya uwanja. 

Brazil itakabiliana na Uswisi kwenye mechi yake ya kwanza siku ya Jumapili, na mabingwa watetezi  Ujerumani itaanza kampeni yake kwa mpambano dhidi ya Mexico siku hiyo hiyo ya Jumapili. Brazil walikuwa wakisubiri kwa hamu kupona kwa Neymar, baada ya kufanyiwa upasuaji Aprili 3, lakini hata hivyo mchezaji huyo ghali zaidi duniani amefunga mabao kwenye mechi mbili za mwisho za kupasha moto misuli.

Urusi inayoandaa michuano hii hata hivyo bado imegubikwa na hofu kubwa, kuhusu iwapo timu yao itawaabisha mbele ya mabilioni ya mashabiki wa soka ulimwenguni. Wenyeji wamevunja rekodi zilizowekwa na Urusi na uliokuwa muungano wa Kisovieti kwa kutoshinda mechi saba na kuanguka hadi nafasi ya 70, hii ikimaanisha kwamba hakuna kocha anayekabiliwa na shinikizo kubwa  kama Stanislav Cherchesov wa Urusi.  Kwa jumla macho na masikio ya wapenzi wa kandanda dunia yanaelekezwa nchini Urusi.

Mwandishi: Lilian Mtono/.AFPE/DPAE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW