1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macho yaelekezwa kwa Afcon Cameroon

3 Januari 2022

Kuanzia tarehe 9 mwezi huu macho yote yataelekezwa nchini Cameroon, kwa mashindano maarufu ya kandanda barani Afrika. Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON inang’oa nanga nchini humo licha ya janga la corona

Kamerun Jaunde | Africa Cup of Nations
Picha: Kepseu/Xinhua/imago images

Viongozi wa kandanda Afrika pamoja na waandalizi wamehakikisha kuwa michezo hiyo itafanyika kama ilivyopangwa, chini ya kanuni kali za kuzuia maambukizi ya corona.

Lakini sio kitisho cha corona tu kinachosababisha tumbo joto. Hali ya mkoa wa kusini magharibi mwa Cameroon ulioharibiwa kwa machafuko inatishia usalama wa mashindano hayo. Wanamgambo wa Eneo hilo wameahidi kuvuruga mashindano hayo.

Cameroon inaandaa mashindano hayo katika miji sita, lakini kuna kitisho kikubwa katika mji wa Limbe, ambao eneo linalouzunguka limekumbwa na mashambulizi ya watu wenye silaha tangu vita vilipozuka mwaka wa 2017.

Kwa sasa magari ya kijeshi yameweka doria mitaani. Honore Kuma ni mwandishi wa habari wa eneo hilo na anasema machafuko yameongezeka mwaka huu "Hofu yangu, hofu ya wakaazi wa Limbe ni kuwa muenendo wa karibuni wa miripuko ya mabomu ambayo imekuwa ikitokea katika maeneo mengine ya eneo la Fako kama Buea huenda ukawa muenendo wa kawaida wakati wa mashindano ya AFCON."

Uwanja wa michezo wa Limbe Omnisport utakuwa mwenyeji wa mechi za Kundi F zinazozijumuisha Tunisia, Mali, Mauritania na Gambia. Mechi ya kwanza ya Kundi hilo ni kati ya Tunisia na Mali Januari 12.

Emmanuel Ledoux Engamba ni afisa mwandamizi wa utawala katika eneo hilo na anaahidi hakutakuwa na tatizo la kiusalama "Ni kwa muktadha huo ndipo tulifaulu kuandaa mashindano ya CHAN miezi michache iliyopita. Kwa hiyo, siwezi kufichua hapa hatua ambazo zinachukuliwa lakini unapaswa kujua kuwa kama tu mechi za CHAN zilivoandaliwa chini ya mazingira mazuri sana, AFCON pia itafanyika chini ya mazingira mazuri kabisa. Hakuna wasiwasi. Hakuna cha kutia wasiwasi." Amesema Engamba

Mzozo huo, ambao makundi yenye silaha yanajaribu kuunda taifa huru la Ambazonia, yamewauwa karibu watu 3,000 na kuwalazimu karibu milioni moja kukimbia makaazi yao.

Reuters