Macky Sall ashinda nchini Senegal
26 Machi 2012Katika uchaguzi wa Rais nchini Senegal Rais Abdoulaye Wade amekubali kushindwa.
Televisheni ya serikali imearifu kwamba Rais huyo mwenye umri wa miaka 85 alimpigia simu kiongoziwa upinzani Macky Sall na kumpongeza kwa ushindi, baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba Sall ameshinda kwa kura 30,000 wakati Wade amepata kura 11,000
Maalfu ya watu wamesherehekea ushindi wa Macky Sall katika mitaa ya mjini Dakar mapema asubuhi.
Watu hao walianza kusherehekea hata kabla ya Rais Wade kukubali kushindwa.Vyombo vya habari vya serikali nchini Senegal vimeshaanza kutoa mfululizo wa matokeo ya uchaguzi uliofanyika hapo jana.
Hofu kwamba Rais Wade angelijaribu kung'ang'ania madaraka au kuyapinga matokeo ya uchaguzi ilisababisha mapambano mabaya katika siku za kuelekea kwenye uchaguzi. Wanaharakati wa upinzani walisema hatua ya Wade ya kugombea muhula wa tatu wa Urais ilikuwa kinyume na katiba.Matokeo rasmi ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa mnamo kipindi cha saa 48.
Mwandishi:Mtullya Abdu/AFP,AP,Reuters
Mhariri: A.Schmidt