Macron aahirisha ziara Ujerumani kutokana na ghasia Ufaransa
1 Julai 2023Ghasia hizo zilichochewa na kuuliwa kwa kupigwa risasi kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 na polisi wa barabarani. Ofisi ya rais wa Ujerumani imetangaza kuwa Macron amezungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na kumfahamisha kuhusu hali nchini mwake, wakati akiomba ziara yake iliyopangwa kuanza kesho Jumapili iahirishwe.
Soma pia:Ghasia zaendelea Ufaransa, zaidi ya watu 1,300 wakamatwa
Polisi waliwakamata watu 1,311 usiku wa kuamkia leo Jumamosi, ikiwa ni idadi kubwa kabisa tangu maandamano yenye vurugu yalipoanza kuhusiana na kuuliwa kwa Nahel M. katika kitongoji cha Paris, cha Nanterre Jumanne wiki hii. Maduka yaliporwa na majumba na magari kuchomwa moto kote nchini licha ya wizara ya mambo ya ndani kuwabwaga mitaani polisi 45,000 na magari ya kivita. Ibada ya mazishi ya Nahel imefanywa katika kintongoji alichoishi cha Nanterre huku umati mkubwa ukijitokeza katika eneo la makaburi.