Macron afanya mazungumzo na viongozi wa upinzani
21 Juni 2022Mikutano hiyo kwenye Ikulu ya Elysee inafanyika baada ya Waziri Mkuu wa Ufaransa Elisabeth Borne kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu mapema leo kama sehemu ya utamaduni wa kawaida pindi uchaguzi wa Bunge unapomalizika.
Hata hivyo rais Macron amekataa kujiuzulu kwa mwanasiasa huyo na kuamuru serikali yake ibakie madarakani. Muungano wa kiliberali wa rais Macron wa Ensemble au "Pamoja" ulishinda viti 245 katika uchaguzi wa Bunge wa siku ya Jumapili. Idadi hiyo ni pungufu ya viti 44 vilivyohitajika ili kuuwezesha muungano huo kuwa na wingi wa viti bungeni.
Muungano wa wanasiasa wa mrengo wa shoto wa Nupes umeshinda viti 131 na kuwa upande wa upinzani wenye nguvu ndani ya chombo hicho cha juu cha kufanya maamuzi nchini Ufaransa. Wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia wameambulia nafasi 89 ya viti katika bunge hilo la Ufaransa lenye jumla ya viti 577.
Hii leo Jumanne Macron anatazamiwa kukutana na wajumbe wa upande wa upinza ikiwemo rais wa chama cha Republicans Christian Jacob, mkuu wa chma cha kisoshalisti Olivier Faure na kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen.
Kuna mikutano mengine kati ya kiongozi huyo na maafisa wengine ambayo haijawekwa wazi. Macron pia amepangiwa kukutana na wawakilishi wa chama chake na washirika wa vuguvugu la kisiasa aliloliunda.
Je, atafanikiwa kutanzua kiwingu kinachoikabili serikali yake?
Mazungumzo hayo yananuwia kutafuta "njia mwafaka" za kutatua mkwamo uliopo kuhusu hatma ya serikali anayoiongoza. Macron mwenyewe bado hajatoa maoni yake hadharani kuhusu uchaguzi wa bunge.
Chama chake ambacho ndiyo kina wabunge wengi bado kinaweza kuongoza serikali lakini kitalazimika kufikia makubaliano na wabunge wengi kupitisha maamuzi au miswada ya sheria.
Ili kuepusha mkwamo unaoweza kujitokesha siku zinazokuja, chama cha Macron na washirika wake wanajadiliana na wanasiasa wengine ili kuona maeneo wanayoweza kufanya kazi pamoja na kuungana mkono.
Macron alichaguliwa kwa muhula wa pili mnamo mwezi Aprili chini ya ahadi ya kuongeza uwezo wa kifedha wa raia mmoja mmoja nchini Ufaransa, kupunguza kodi na kupandisha umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 65.
Baadhi ya wanasiasa wasema wako tayari kuunga mkono baadhi ya sera za Macron
Wakati akielekea kwenye ukumbi wa mikutano kwenye Ikulu ya Elysee, Jacob amesema chama cha Republicans chenye viti 61 kitabakia upande wa upinzani na haitoingia kwenye "makubaliano au muungano" wowote na waliberali wa Macron.
Hata hivyo amesema watakuwa tayari kuunga mkono baadhi ya sera zinazokwenda sambamba na ajenda ya chama chao. Amesema masuala kama mabadiliko ya pensheni ni sehemu ya ajenda wanazopigia upatu sawasawa na chama cha Macron.
Kiongozi wa Wasoshalisti, Olivier Faure aliwaambia waandishi habari kwamba "kuna uwezekano wa kusonga mbele pamoja lakini hatutaunga mkono sera zitakazokwenda kinyume na ahadi tulizowapatia Wafaransa".