1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUfaransa

Macron ahimiza mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa

22 Juni 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amefungua mkutano wa kilele wa siku mbili mjini Paris. Mkutano huo unafanyika wakati dunia inakabiliwa na hali mbaya ya hewa na changamoto zingine za kimaendeleo

Frankreich | Internationaler Gipfel für einen neuen globalen Finanzpakt in Paris
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais wa Ufaransa Emanuel Macron amewakaribisha viongozi wa dunia na wataalam mjini Paris kwenye mkutano huo wa kilele wa hali ya hewa unaofanyika kwa siku mbili leo Alhamisi hadi kesho Ijumaa. Mkutano huo wa kilele wa hali ya hewa unalenga kuweka mikakati ya kupunguza mizigo ya madeni ya nchi zenye kipato cha chini, na wakati huo huo kutenga fedha zaidi za ufadhili wa majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Viongozi kadhaa wanaohudhuria mkutano huo katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris wanalenga kufikia makubaliano ya ngazi ya juu kuhusu jinsi ya kuendeleza mipango kadhaa ambayo kwa sasa inaning'nia katika mashirika kama ya G20, Shirika la Fedha duniani- IMF, Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa.

Kushoto: Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa. Kulia: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Picha: Ludovic Marin/REUTERS

Mada nyingi katika ajenda zimechukuliwa kutoka kwenye mapendekezo ya kundi la nchi zinazoendelea, linaloongozwa na Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley, lililopewa jina la 'Mpango wa Bridgetown' unaojumuisha maswala kuhusu misamaha ya madeni hadi fedha za kufadhili mipango ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akiufungua mkutano huo Rais Macron amewaambia viongozi wa kimataifa kwamba wanapotafakari upya mfumo wa fedha duniani, hakuna nchi itakayoshinikizwa kuchagua kati ya kukabiliana na umaskini au kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley alipokuwa kwenye mkutano wa COP27 nchini Misri.Picha: Dominika Zarzycka/NurPhoto/picture alliance

Wajumbe katika mkutano huo wa kilele unaojadili juu ya kupatikana mkataba mpya wa kimataifa wa maswala ya fedha pia unalenga kutafuta suluhu za kifedha kwa malengo ya kimataifa ya kukabiliana na umaskini, kuzuia joto kali katika sayari na kufanikisha malengo ya kulinda hali asilia.

Mwanaharakari mmoja wa mazingira Vanessa Nakate amesema kwenye mkutano huo kwamba kutokana na uchu wa nishati dunia inashuhudia watu wanavyopoteza njia za kumudu maisha yao na wengine wanapoteza maisha yao.

Ingawa maamuzi kamilifu hayatarajiwi kwenye mkutano huo, maafisa wanaohusika katika kuupanga mkutano huo wameisema wana imani baadhi ya ahadi zitashughulikiwa hasa kuhusu kuzifadhili nchi maskini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewwambia wajumbe kwenye mkutano huo wa kilelele kwamba mashirika ya fedha ya kimataifa kwa sasa yamenywea na kuwa madogo mno kiasi cha kushindwa kutimiza wajibu wa mashirika hayo.

Vyanzo: AP/RTRE/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW