1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron akosolewa kumkaribisha rais al-Sisi wa Misri

8 Desemba 2020

Rais Emmanuel Macron ameipinga mitizamo ya kukosoa ushirikiano wake wa karibu na rais wa Misri AbdelFatah Al Sisi,akisema kwamba kuchukua msimamo mkali kuhusu suala la kuheshimu haki za binadamu itakuwa sio hatua bora.

Frankreich Paris | Treffen | Macron und al-Sisi
Picha: Eliot Blondet/ABACA/picture alliance

Rais Emmanuel Macron ni mwenyeji wa ugeni wa kiongozi huyo wa Misri Abdul Fatah al Sisi aliyeitembelea Ufaransa katika ziara ya kiserikali ya siku tatu. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika siku ya pili ya ziara ya Al sisi amemtaja kiongozi huyo wa Misri kuwa ni rafiki yake na amekosoa miito ya wale wanaomtaka achukue msimamo mkali kuelekea Misri kuhusu suala zima la ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ziara hii ya Al Sisi ni ya mazungumzo na mwenyeji wake. Mashirika ya kutetea haki za binadamu, Amnesty International na mengineyo yameikosoa na kuishutumu Ufaransa kwa kumkaribisha rais huyo wa Misri ambaye kwa muda mrefu ameendesha ukandamizaji wa kikatili kwa upinzani wa aina yoyote nchini mwake na kumwambia bwana Macron kwamba wakati ni sasa wa kusimama kutetea haki za binadamu na hakuna wakati mwingine.

Rais Macron na mgeni wake rais wa Misri al-SisiPicha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo rais huyo wa Ufaransa amejizuia kumkosoa moja kwa moja jenerali huyo wa zamani wa jeshi la Misri, Al Ssisi ambaye amekuwa akiwaandama wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani ambaye sasa ni Marehemu Mohammed Morsi sambamba na wafuasi wa mrengo wa shoto na wakiliberali nchini Misri.

Katika mkutano na waandishi habari pamoja na viongozi hao wawili wa nchi, Macron amewaambia waandishi kwamba amelizungumzia suala la haki za binadamu wakati wa mazungumzo yao na Al Sisi na amesema amebakia kuwa mtetezi asiyebadilika wa uwazi wa kidemokrasia na kijamii.

Lakini ameondowa uwezekano wa kulitumia suala la ushirikiano mkubwa wa Ufaransa wa kijeshi na Misri kuwa sharti katika suala hilo la haki za binadamu.

Badala yake Macron amesema anafikiri ni bora zaidi kuwa na sera ya mazungumzo kuliko kufuata sera ya kususia ambayo itapunguza uwezo wa mmoja wa washirika wao katika mapambano dhidi ya ugaidi na uthabiti na usalama wa kikanda.

Nchi zote ambazo zina wasiwasi sawa kuhusu ukosefu wa uthabiti katika eneo zima la Sahel, vitisho vya makundi ya kigaidi ya Jihad pamoja na mwangwi wa kisiasa nchini Libya, wameonekana kuimarisha uhusiano wa karibu wa kiuchumi na kijeshi na nchi hiyo ya Misri chini ya rais Abdel Fatah al sisi.

Karibu Ufaransa al-SisiPicha: Eliot Blondet/ABACA/picture alliance

Ingawa ndani ya Ufaransa kwenyewe miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu kuna wenye wasiwasi mkubwa kuhusu hatua ya Macron ya kumkumbatia al Sisi ambaye amekwenda Ufaransa wakati maelfu ya wapinzani wake wamefungwa jela. Kwa upande mwingine rais huyo wa Misri anazipinga kauli zinazomkosoa na kumshutumu juu ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Al Sisi amesema sio sawa hata kidogo kuiangalia serikali ya nchi hiyo na kila kitu inachokifanya kwa watu wake na kwa uthabiti wa kanda hiyo kama utawala wa ukandamizaji.

Ama kuhusu suala lililozusha hasira katika ulimwengu wa nchi za kiislamu la kuchapishwa kwa vitakatuni vya mtume Mohammed Macron kwa mara nyingine ametetea uhuru wa kujieleza akisema ni msingi wa maadili ya Ufaransa lakini rais al Sisi wa Misri hakuchelea kumpinga mwenyeji wake akisema maadili ya binadamu yametengenezwa na binadamu na siku zote yanaweza kubadilishwa lakini maadili ya dini ni kitu kitakatifu kuliko kitu chochote kile.

Kiongozi huyo wa Misri amesema ikiwa kujieleza kwa mtu kunaumiza hisia za mamia ya mamilioni ya watu na unadhani kwamba hicho hakiwezi kubadilishwa basi itahitaji kufikiria zaidi na kuiangalia nafsi yako.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW