Macron amfungulia kesi mshawishi wa mtandaoni Candace Owens
24 Julai 2025
Kesi hiyo inahusu kashfa ambayo Owens alidai kwamba mke wa rais huyo alizaliwa mwanaume.
Owens alitoa madai hayo, miongoni mwa mengine dhidi ya wanandoa hao wa Ikulu ya Ufaransa, kupitia mtandao wa X na katika kipindi chake mnamo Machi 2024.
Kesi hiyo ya kisheria, ambayo Owens mwenyewe alithibitisha kupitia video ya YouTube, inamshutumu kwa kutoa "kauli hii ya uongo ili kujinufaisha kupitia jukwaa lake binafsi, kujitafutia umaarufu, na kupata fedha."
Miongoni mwa madai hayo ni kwamba Brigitte na Emmanuel Macron ni ndugu wa damu, na kwamba Emmanuel Macron alipata urais kwa msaada wa mpango maalum wa shirika la kijasusi la Marekani (CIA).
Kesi hiyo inasema kuwa Macron na mkewe wamekuwa wahanga wa "kampeni ya kuaibishwa duniani kote na isiyo na msingi wowote." Owens amekuwa akizua utata mara kadhaa kutokana na misimamo yake. Mnamo 2024, serikali ya Australia ilimkatalia kuingia nchini humo, ikitaja kusambaza kwake madai ya uongo kuhusu mauwaji ya Holocaust na Waislamu.