1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron amsifu Abiy kwa mageuzi ya kihistoria Ethiopia

Mohammed Abdulrahman
30 Oktoba 2018

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amempongeza waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kwa utekelezaji wa sera yake ya mageuzi yenye lengo la kuleta mabadiliko katika taifa hilo la pembe ya Afrika.

Frankreich Emmanuel Macron und Abiy Ahmed
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akishikana mikono na waziri mkuu Ahmed Abiy wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Paris, Okotoba 29, 2018.Picha: Getty Images/AFP/M. Euler

Rais  Emmanuel Macron ameyataja mageuzi ya waziri mkuu huyo kijana mwenye umri wa miaka 42 kuwa yasiyotarajiwa. Abiy yuko katika ziara yake ya kwanza  barani ulaya  tangu aliposhika wadhifa huo mwezi Aprili  baada ya kujiuzulu ghafla mtangulizi wake Hailemariam Desalegn mwezi Februari..

Amepongezwa  takriban na wengi  ulimwenguni kwa jitihada zake za kuleta amani na taifa jirani la Eritrea, kutangaza mageuzi ya kuchumi na kuwanyooshea mkono wa  maridhiano wapinzani ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru  maelfu ya wafungwa wakiwemo  wa kisiasa, kuviruhusu  tena vyama vya kisiasa vilivyopigwa marufuku  na kuahidi uchaguzi huru na wa haki  2020,  ingawa bado  anakabiliana na  mizozo ya  kikabila iliosababisha watu milioni 1.4 kuyahama makazi yao.

Akizungumza  katika mkutano na waandishi habari mjini Paris akiwa pamoja na kiongozi huyo wa Ethiopia, Rais Macron alisema Ufaransa inaziunga mkono juhudi zake za  kuleta  mabadiliko nchini Ethiopia na akamwambia Dr Abby, "hapa una nchi inayoipenda nchi yako na kuvutiwa pia na mageuzi unayoyatekeleza."

Waziri mkuu wa Ethiopia Dk. Abiy Ahmed akipokelewa katika ikulu ya Elysee, na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.Picha: DW/H. Tiruneh

Macron akaongeza kusema kwamba  anafahamu changamoto kubwa aliyokabiliana nayo  Waziri mkuu Abiy katika kuleta mabadiliko hayo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, akisema ni jambo lisilo tarajiwa.

Ufumbuzi kupitia amani na maridhiano

Kwa upande wake kiongozi huyo wa Ethiopia aliahidi kutatua migogoro  na mapigano ya kikabila , akisema ufumbuzi utapatikana kwa maridhiano na kupigania amani na anaamini mabadiliko yataleta suluhisho." 

Akamtaka Macron kutoa mchango mkubwa  katika juhudi za kuimarisha amani kati ya  Eritrea na Djibouti, ambazo  zilikubaliana mwezi uliopita  kurejesha uhusiano wao katika hali ya kawaida baada ya  muongo mmoja wa  mzozo wa mpaka  uliosababisha mapigano ya muda mfupi kati yao.

Ufaransa na Ethiopia zimesaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika nyanja  mbali mbali kuanzia usafiri hadi nishati na  utamaduni.

Waziri mkuu Abiy Ahmed, amegeuza nchi yake Ethiopia kuwa ya kwanza barani Afrika, kuleta  mageuzi ya uongozi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika baraza la mawaziri , idadi sawa kati ya wanaume na wanawake. Mnamo wiki iliopita  wabunge  mjini Addis Ababa  walimuidhinisha  rais wa kwanza  mwanamke  nchini humo, na ambaye kwa wakati huu ndiye mkuu pekee wa taifa aliye mwanamke barani Afrika .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ap,afp

Mhariri: Yusuf, Saumu