Macron asema Ufaransa ingeweza kusitisha mauaji Rwanda
5 Aprili 2024Ofisi ya Macron imesema katika taarifa kwamba rais wa Ufaransa atatoa video kwenye mitandao ya kijamii Jumapili ijayo wakati Rwanda ikifanya kumbukumbu ya miaka 30 ya mauaji hayo. Kwenye video hiyo Macron anasema kwamba Ufaransa, ambayo ingeweza kuepusha mauaji hayo pamoja na washirika wake wa Magharibi na Afrika, ilikosa ari ya kufanya hivyo.
Mnamo 2021 wakati wa ziara yake nchini Rwanda, rais Macron alitambua wajibu wa Ufaransa katika mauaji hayo ambapo watu 800,000 walikufa, wengi wao wa jamii ya Tutsi na WaHutu waliojaribu kuwalinda. Hatua ya hivi sasa ya Rais Macron imepongezwa nchini Rwanda na vilevile nchini mwake Ufaransa.
''Ufaransa imechukuwa hatua muhimu sana''
Vicent Duclert aliyeongoza tume ya wanahistoria wa Ufaransa ili kuchunguza wajibu wa Ufaransa katika mauwaji ya kimbari ya Rwanda amesema kauli ya rais Macron ni ukweli usiopingika.
"Umma wa Ufaransa umegundua kile ambacho watu wengi tayari wanajua na wamefikia ukweli wa kihistoria. Ninamaanisha, hakujawa na shida ya kumbukumbu nchini Ufaransa. Kinyume chake, ningesema kulikuwa na hali ya utulivu. Ni kweli kwamba ukweli huponya na hata kukufanya ukue na hapa, nadhani, Ufaransa imechukuwa hatua muhimu sana.'', alisema Duclert.
Kipi kifanyike ?
Hata hivyo rais Emmanuel Macron hatahudhuria tukio hilo la kumbukumbu ya miaka 30 ya mauwaji ya kimbari ya Watutsi wa Rwanda. Atawakilishwa Jumapili mjini Kigali na Waziri wa Mambo ya Nje, Stéphane Séjourné, na naibu waziri wake, Hervé Berville.
Kundi la Ibuka linalowawakilisha watu walionusurika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 limesifu tangazo la rais Macron. Marcel Kabanda, kiongozi wa kundi hil nchini Ufaransa amesema amefurahishwa na kile anachokiita kama hatua muhimu ambayo imeckuliwa na Ufaransa. Anatoa wito kwa Ufaransa kwenda mbali zaidi kwa kuwaomba radhi wahanga wa mauaji hayo ya kimbari.
Wahusika wawajibishwe
Aidhaa mashirika yanayofuatilia kuwajibishwa kwa watu waliohusika na mauwaji ya kimbari nchini Rwanda yanamaoni tofauti. Mashirika hayo yamesema ni hatua ndogo iliofikiwa na Urafansa, huku yakiitaka nchi hiyo kuchukuwa hatua zaidi.
Aprili 7 mwaka huu, Rwanda inaadhimisha miaka 30 tangu kutokee mauaji ya kimbari ambayo yalisababisha vifo vya karibu watu 800,000 wengi wao wakiwa ni Watutsi.