Macron asema Uturuki ni mshirika muhimu
7 Septemba 2017Uturuki na Ujerumani ambao ni washirika katika Jumuiya ya NATO wameshambuliana kwa maneno makali, katika muda wa miaka miwili . Lakini Umoja wa ulaya kwa jumla umeshitushwa na hatua za ukandamizaji za rais Tayyip Erdogan dhidi ya wapinzani kufuatia jaribio lililoshindwa la mapinduzi nchini Uturuki Julai mwaka jana.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliimarisha msimamo mkali kuhusiana na juhudi za Uturuki zilizokwama kwa muda mrefu katika mdahalo wa televisheni Jumapili iliyopita pamoja na mgombea mwenzake katika uchaguzi wa taifa unaotarajiwa kufanyika Septemba 24.
Afisa mwandamizi wa Uturuki amesema mataifa ya Umoja wa Ulaya yanapaswa kuamua iwapo wanaitaka Uturuki kuwa mwanachama ama la, lakini kuna hisia "kwamba hawataki tena ndoa , bali wanataka kuishi pamoja tu.
Matamshi ya rais wa Ufaransa Macron yanafuatia matamshi ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kusitisha kabisa mazungumzo na Ankara.
"Ni kweli kwamba Uturuki imetoka nje ya njia ya Umoja wa Ulaya katika miezi ya hivi karibuni na kinachotia wasi wasi zaidi ni ukiukaji kwa njia ambayo haiwezi kupuuzwa," Macron ameliambia gazeti la Ugiriki la Kathimerini.
"Lakini nataka kuepuka kuvunjika, kwasababu ni ni mshirika muhimu katika mizozo mingi ambayo tunakabiliana nayo, hususan changamoto za uhamiaji na kitisho cha ugaidi."
Makubaliano na Uturuki
Umoja wa Ulaya unahaja ya kulinda makubaliano na Uturuki ambayo yametokana na wimbi la wahamiaji kupitia ardhi ya Uturuki la watu kutoka katika maeneo ya mizozo. Uturuki hapo nyuma iliwahi kuhoji nia thabiti ya Umoja wa Ulaya ya kutekeleza upande wake wa makubaliano.
Mahusiano kati ya Ankara na Umoja wa Ulaya yameporomoka tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi Julai mwaka 2016 ambalo lilifuatiwa na hatua za kukamatwa kwa maelfu ya watu nchini humo. Wakosoaji wanamshutumu rais Recep Tayyip Erdogan kwa kutumia kisingizio cha mapinduzi kuwabana wapinzani wa kisiasa.
Uturuki ambayo ilitia saini makubaliano ya ushirika na Umoja wa ulaya mwaka 1963, ilianza majadiliano rasmi ya kujiunga na Umoja huo mwaka 2005. Hata hivyo , wanachama kadhaa , ikiwa ni pamoja na Ufaransa , wamepinga mazungumzo hayo ama baadhi ya vipengee ikiwa na maana kwamba ni sura 16 tu za majadiliano kati ya 35 zimekwisha funguliwa.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Finland na Lithuania wamezungumzia pia dhidi ya kutovunja mazungumzo na Uturuki.
"Hapana, tunapaswa kuendelea na mchakato wa mahusiano. sio rahisi lakini tunapaswa kuthamini mahusiano," waziri wa mambo ya kigeni wa Lithuania Linas Linkevicius amewaambia waandishi habari.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu