1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Macron ashikilia mageuzi ya pensheni kufanyika Ufaransa

22 Machi 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumatano amesema kwamba muswada wa pensheni aliousukuma na kuupitisha bila kupigiwa kura bungeni unahitaji kutekelezwa ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Frankreich Rentenreform Streik
Picha: LUDOVIC MARIN/AFP

Macron aliyetoa matamshi hayo katika mahojiano yaliyorushwa kwenye televisheni ya taifa nchini Ufaransa, amesema muswada huo unaoongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64, utaendelea na kile alichokiita "njia yake ya kidemokrasia" kwani Baraza la Katiba litauangazia katika wiki chache zijazo.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa rais huyo kuzungumza hadharani tangu serikali yake ilipoupitisha muswada huo bungeni, wiki iliyopita. Katika mahojiano hayo, Macron mwenye umri wa miaka 45 amesema mara kadhaa kwamba ana uhakika mfumo wa kustaafu nchini humo unastahili kufanyiwa mageuzi ili kuhakikisha kwamba una fedha.

"Unafikiri nafurahia kufanya mageuzi haya? Hapana. Ila hakuna njia nyengine ya kusawazisha masuala ya fedha, kwa hiyo mageuzi yanahitajika," alisema Macron.

Imani kwa waziri Mkuu Borne bado ipo

Vile vile Macron ambaye katiba ya Ufaransa haimruhusu kugombea muhula wa tatu anasema yuko radhi kukabiliana na upinzani wowote utakaotokana na mageuzi hayo ya mfumo wa pensheni.

Polisi wakimkabili mwandamanaji katika mji wa Rennes JumatanoPicha: Jeremias Gonzalez/AP Photo/picture alliance

Aidha, kiongozi huyo wa Ufaransa amekataa mwito wa upinzani wa kumtaka amuachishe kazi Waziri Mkuu Elisabeth Borne kutokana na jinsi serikali ilivyolishughulikia suala hilo la mageuzi katika mfumo wa pensheni. Macron amesema bado ana imani na huyo waziri wake mkuu.

Uamuzi wa Macron wiki iliyopita wa kutumia nguvu za kikatiba alizo nazo kuupitisha muswada huo bungeni bila kupigiwa kura na wabunge ni jambo lililowagadhabisha wengi bungeni na kote nchini humo.

Utafiti wa maoni unaonyesha kwamba idadi kubwa ya Wafaransa wanaipinga sheria hiyo. Mashirika ya wafanyakazi yametangaza migomo na maandamano hapo kesho kote nchini humo.

Kuelekea mahojiano hayo ya Jumatano, waandamanaji walijitokezakatika mitaa ya miji ya kusini mwa Ufaransa ya Nice na Toulouse ambapo waliweka vizuizi katika malango ya kuingia kwenye vituo vya treni.

Usalama katika ziara ya Mfalme Charles III umashakani

Huko Marseille wafanyakazi wa bandari walifunga malango ya kuingia bandari ya mji huo ambayo ndiyo bandari kubwa zaidi nchini Ufaransa, jambo lililozuia malori na magari kuingia huku kukiwa na uwepo mkubwa wa maafisa wa polisi.

Mwandamanaji akiwarushia polisi mkebe wa moshiPicha: Jeremias Gonzalez/AP Photo/picture alliance

Katika baadhi ya mitaa ya mji mkuu Paris, taka zimeendelea kurundikana wakati ambapo wafanyakazi katika idara ya usafi wakiwa wameingia katika siku yao ya kumi na saba ya mgomo.

Hivi majuzi, mamlaka nchini humo zilitoa amri ya kuwataka baadhi ya wafanyakazi katika idara hiyo kufanya kazi kidogo tu, kwa ajili ya sababu za kiafya.

Migomo hii pamoja na mwingine unaoathiri hifadhi za mafuta ni mambo yanayoonyesha changamoto kubwa inayoikabili serikali ya rais huyo tangu yale maandamano ya vizibao vya njano miaka minne iliyopita.

Mivutano hii nchini Ufaransa imeibua maswali ya uwezo wa Ufaransa kuwa mwenyeji wa Mfalme Charles wa III wa Uingereza atakapowasili Jumapili katika ziara yake ya kwanza ya kigeni katika utawala wake.

Vyanzo: AP/AFP/Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW