1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Macron ataka wanasiasa kuungana dhidi ya misimamo mikali

Sylvia Mwehozi
12 Juni 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Marcon amevitolea mwito vyama vya siasa za wastani kutoka mirengo ya kushoto na kulia nchini humo, kuungana pamoja dhidi ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi ujao wa bunge.

 Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Marcon Picha: Michel Euler/AP Photo/picture alliance

Macron, amezungumza na wapiga kura wa Ufaransa kwa mara ya kwanza tangu uamuzi wake wa kushutukiza wa kulivunja bunge la kitaifa na kuitisha uchaguzi wa mapema. Katika mkutano na waandishi wa habari, Macron amesema kuwa aliamua kuchukua uamuzi huo wa hatari kwasababu asingeweza kupuuzia uhalisia mpya wa kisiasa, baada ya chama chake kinachopigia upatu Umoja wa Ulaya, kushindwa vibaya na chama cha siasa kali cha National Rally RN, katika uchaguzi wa bunge la Ulaya. Watu "wanahisi kuwa hawasikilizwi au kuheshimiwa."

Aidha kiongozi huyo amekiri wazi kwamba "hawawezi kuendelea kana kwamba kila kitu kiko sawa" bila ya kuwasikiliza Wafaransa hasa kwa kuzingatia namna wapiga kura walivyokichagua chama cha RN.

Kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Republicans Eric CiottiPicha: Christophe ARCHAMBAULT/AFP

"Hatuwezi kubaki kimya kuhusu ujumbe uliotumwa na wapiga kura na lazima tutoe jibu la kidemokrasia. Tuko katika nyakati ambazo nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi na haiwezi kuruhusu wenye misimamo mikali watuzuie. Kwa mtizamo wangu, kuwageukia watu wetu huru lilikuwa ndio chaguo pekee la kidemokrasia."

Mwanasiasa huyo anajaribu kutafuta muungano dhidi ya vyama vya siasa za itikadi kali katika uchaguzi huo wa mapema na kwamba anakusudia kukizuia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kurithi mikoba yake pindi atakapostaafu mwaka 2027. Pia ameahidi kushughulikia masuala ya uhamiaji, usalama na haki.

"Sitaki kutoa funguo za mamlaka kwa watu wa siasa kali mwaka 2027", amesema Macron akiongeza kuwa anawajibika kikamilifu kwa kuanzisha mchakato huo uliochochewa na tangazo lake la uchaguzi wa mapema.

Macron pia amekikosoa chama cha kihafidhina cha Republican , ambacho kiongozi wake Eric Ciotti alitangaza muungano na chama cha RN sambamba na kambi ya muungano wa kushoto ikiwemo chama cha siasa kali za kushoto cha France Unbowed LFI.

Kiongozi wa kitaifa wa chama cha National Rally Marine Le Pen Picha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Kiongozi wa kitaifa wa chama cha National Rally RNMarine Le Pen anajaribu kuunganisha nguvu upande wa kulia katika juhudi za kutafsiri ushindi wa bunge la Ulaya kuwa ushindi wa kitaifa na kutwaa mamlaka ya nchi.

Chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia, chenye historia ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni, kinatarajiwa kushinda viti vingi zaidi vya Ufaransa katika Bunge la Ulaya, uwezekano wa viti 30 kati ya 81 vya Ufaransa.

Soma: Macron akosa wingi wa kutosha bungeni

Hata kama chama cha RN kitashinda katika uchaguzi wa Juni 30 na Julai 7, Macron atasalia kuwa rais kwa miaka mitatu zaidi na bado atasimamia ulinzi na sera za kigeni lakini atapoteza udhibiti wa ajenda za  ndani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW