1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron atangaza mkakati kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi

Yusra Buwayhid
21 Februari 2019

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza Jumatano serikali yake itatumia ufafanuzi wa kimataifa kuhusu suala la chuki dhidi ya Wayahudi, na kuwasilisha muswada mpya wa kukabiliana na matamshi ya chuki mtandaoni.

Frankreich Rede Emmanuel Macron - Antisemitismus in Frankreich
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Marin

Akizungumza wakati wa chakula cha jioni mbele ya wanachama wa mwamvuli wa mashirika ya kiyahudi nchini Ufaransa (CRIF), Macron alisema kwamba muswada sawa na huo tayari unatumika kiufanisi nchini Ujerumani.

Sheria ya Ujerumani inasema kwamba matamshi ya chuki lazima yaondolewe kwenye tovuti ndani ya masaa 24 baada ya kuripotiwa, na wakati mwengine huenda tovuti hizo zikatozwa hata faini ya mamilioni ya euro.

Macron ameukosoa zaidi mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kutumia siku nyingi, na wakati mwengine hata wiki kadhaa, kuondoa matamshi ya chuki na kuzisaidia mamlaka ili mahakama iweze kuongoza uchunguzi wake. Wakati huo huo, ameusifu uamuzi wa Facebook wa 2018 kuruhusu kuwepo kwa wasimamizi wa Kifaransa ndani kampuni hiyo ili kusaidia kuboresha njia za kupambana na matamshi ya chuki mtandaoni.

Rais huyo wa Ufaransa pia amesema amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Christophe Castaner, kuyasambaratisha makundi yanayochochea chuki na vurugu nchini humo.

Macron aukemea mtandao wa Twitter

Mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi, yameongezeka nchini Ufaransa hivi karibuni kwa asilimia 74 ndani ya mwaka 2018, na kufika hadi visa 541.

Emmanuel Macron akitembelea Quatzenheim eneo la makaburi ya Kiyahudi yaliyochorwa nembo za KinaziPicha: Reuters/F. Florin

Macron amesema kwa kutumia ufafanzui huo wa suala la chuki dhidi ya Wayahudi ambao unatumiwa tayari na Ushirikiano wa Kimataifa wa Kumbukumbu wa Mauaji ya Holocaust kutasaidia kuviongoza vikosi vya polisi, mahakimu na walimu katika kazi zao za kila siku.

"Upinzani dhidi ya kuundwa kwa taifa la Kiyahudi katika Mashariki ya Kati ni mojawapo ya aina za kisasa za kuonyesha chuki dhidi ya Wayahudi. Hivyo ndiyo maana, ninahakikisha kwamba Ufaransa, ambayo kama mlivyoikumbusha, imependekeza Desemba iliyopita na washirika wake wa Ulaya, itaweka wazi ufafanuzi wa kitendo cha chuki dhidi ya Wayahudi kama inavyoainishwa na Muungano wa Kimataifa wa Kumbukumbu ya mauaji ya Holocaust," amesema Macron.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemshukuru Macron kwa njia ya simu kabla ya hotuba yake hiyo, kwa kuamua kutumia ufafanuzi wa kimataifa wa suala la chuki dhidi ya Wayahudi.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa,ap

Mhariri: Bruce Amani

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW