1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Macron atoa wito wa vikwazo vya kimataifa kwa Iran

14 Novemba 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ametoa wito wa kuwekewa vikwazo vya kimataifa kwa maafisa wa Iran kutokana na ukandamizaji wa serikali kwa vuguvugu la waandamanaji alilolitaja kwa mara nyingine kuwa "mapinduzi".

Spanien | NATO Gipfel in Madrid Emmanuel Macron
Picha: Christophe Ena/AP Photo/picture alliance

Macron ametoa wito huo wa vikwazo vya kimataifa Jumatatu ( 14.11.2022) wakati wa mahojiano na kituo cha redio cha France Inter baada ya kuwakasirisha maafisa wa Iran siku ya Ijumaa kwa kukutana na wanawake wanne mashuhuri wa nchi hiyo ambao wameunga mkono kwa dhati maandamano ya miezi miwili, ambayo yamekuwa changamoto kubwa kwa jamhuri hiyo ya Kiislamu tangu kuondolewa madarakani shah mwaka 1979.

Macron aunga mkono hatua za kidiplomasia

Wakati wa mahojiano hayo, Macron amesema anaunga mkono hatua madhubuti za kidiplomasia na vikwazo dhidi ya maafisa wa serikali ambao wamehusika katika ukandamizaji wakati wa maandamano hayo. Macron ametaja ukandamizaji huo kuwa wa aina yake na ambao haujawahi kutokea na kusema kwamba hawapuuzi chaguo lolote huku akibainisha kuwa serikali ya Iran tayari ilikuwa ikilengwa na vikwazo vingi. Macron ameongeza kuwa ni wanawake walioanzisha maandamano hayo na kwamba wajukuu wa wanamapinduzi wa Kiislamu sasa wanafanya maandamano.

Macron pia amesema, jambo la kuvutia zaidi katika vuguvugu hilo, ni kwamba linawahusisha vijana wa kike na wa kiume ambao hawajawahi kujua chochote zaidi ya utawala uliopo. Wizara ya mambo ya nje ya Iran imeyataja matamshi ya Macron baada ya kukutana na wanawake hao kuwa kile iliyoyaita ya kusikitisha na ya aibu.

Rais wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Wanaharakati walikuwa wamekosoa vikali uamuzi wa Macron kukutana na Rais wa Iran Ebrahim Raisi pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, wakati alikuwa akitafuta kufufua makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran. Katika mahojiano yake, Macron alisema ataweka wazi mazungumzo na Raisi lakini akakiri kwamba hali ya sasa imetatiza zaidi mchakato wa mkataba wa nyuklia.

Iran yakabiliwa na duru mpya ya vikwazo

Huku hayo yakijiri, Iran inakabiliwa na duru mpya ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya, baada ya wanadiplomasia wa Ulaya kukubaliana kuiadhibu kutokana na ukandamizaji wake dhidi ya maandamano ya serikali. Haya yamethibitishwa Jumatatu na duru kadhaa za wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwa shirika la habari la dpa. Hatua hizo za kinidhamu zinawaathiri watu na mashirika 31 ikiwa ni pamoja na wawakilishi wakuu wa idara ya polisi na jeshi la Basij.

Akizungumza mjini Brussels nchini Ubelgiji kabla ya kuthibitishwa kwa uamuzi huo, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, amesema vikwazo hivyo vinatuma ishara ya wazi kwa wale waliohusika ambao wanaamini wanaweza kuwadhulumu, kuwatisha na kuwaua watu wao wenyewe bila kuchukuliwa hatua.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW