Macron azindua mageuzi katika sekta ya ajira Ufaransa
31 Agosti 2017Serikali ya Rais Emmanuel Macron imetangaza mipango kabambe ya mageuzi katika sheria za ajira nchini Ufaransa. Mpango huo unajumuisha mageuzi matano makuu kisheria ambapo kwa mara ya kwanza kampuni ndogondogo na za kati zitapewa kipaumbele. Hatua ya Macron inajiri wakati ambapo kura ya maoni inaonesha kuwa umaarufu wake umeendelea kushuka.
Rais Emmanuel Macron mwenye umri wa miaka 39 na mfuasi wa siasa za mrengo wa kati, anayaona mageuzi katika sekta ya ajira nchini Ufaransa kama njia ya kusuluhisha suala la ukosefu wa ajira unaokadiriwa kuwa asilimia 9.5 nchini Ufaransa, takwimu ambazo ni maradufu ikilinganishwa na nchi za Ujerumani na Uingereza.
Udhibiti wa vyama vya wafanyakazi
Mageuzi hayo yanalenga kudhibiti nguvu za vyama vya wafanyakazi, kupunguza ufutwaji wa watu kazini kwa njia isiyo ya haki, na kuwaruhusu mabosi kuelewana na waajiriwa wao kuhusu masharti na mazingira yao ya kazi.
Akiyazindua mageuzi hayo, Waziri Mkuu wa Ufaransa Edourd Philippe amesema yatasaidia Ufaransa kurejesha hali zilizopotezwa kwa miaka mingi ya ukosefu mkubwa wa ajira. Edourd amesema: "Hakuna anayeweza kusema leo kuwa sheria yetu na hususan sheria ya ajira kuwa inapendelea utoaji ajira. Hakuna anayeweza kusema kuwa ni sheria imara inayolinda na kusaidia kukuza maendeleo ya kudumu ya biashara. Labda zamani lakini si sasa. Sheria ya Ajira ilivyo leo ni kizingiti dhidi ya uwekezaji."
Mageuzi hayo yatatekelezwa kupitia amri ya rais, hali itakayomwezesha Macron Kukwepa mijadala mirefu ya bungeni. Yataidhinishwa na serikali mwezi ujao kisha pia yaidhinishwe na bunge ambalo chama cha Macron kina wingi wa viti.
Chama kikuu cha wafanyakazi chaitisha maandamano
Hatua hiyo inatarajiwa kuchochea maandamano ya kwanza dhidi ya serikali yake, huku chama kikubwa cha wafanyakazi CGT na chama kipya cha kisiasa, Unbowed vikiitisha maandamano tarehe 12 na 23 Septemba.
Tangazo la maandamano linajiri wakati uungwaji mkono wa Macron ukiendelea kushuka. Kura za maoni za hivi karibuni zinaonesha kuwa ni asilimia 40 pekee ya Wafaransa wanaoridhishwa na utendakazi wake.
Mageuzi hayo ni muhimu kwa ajenda ya Macron kwa taifa hilo na ni hatua ya kwanza ya mipango yake kubadilisha mfumo wa kijamii nchini Ufaransa, ambayo pia yatajumuisha mageuzi katika malipo ya uzeeni.
Waziri wa kazi Muriel Penicaud amesema mageuzi hayo hayalengi tu kubadilisha sheria, bali pia kubadilisha tabia na maelewano ya kijamii nchini humo.
Mwandishi: John Juma/AFPE/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga