1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron kuongoza mkutano wa ulinzi kuhusu mapinduzi ya Niger

29 Julai 2023

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, leo ataongoza mkutano wa ulinzi kuhusu mapinduzi yaliyotokea Niger, baada ya jenerali mwenye ushawishi kujitangaza kuwa kiongozi mpya.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AFP

Haya ni kwa mujibu wa ofisi ya rais huyo. Macron amelaani vikali hatua ya waasi hao ya kumuondoa madarakani Mohamed Bazoum siku ya Jumatano.

Soma zaidi: Jenerali Abdourahamane Tiane ajitangaza kuwa kiongozi mpya Niger 

Kiongozi huyo wa Ufaransa amesema mapinduzi hayo ya kijeshi ni haramu na ni hatari kwa watu wa Niger, na eneo zima kwa ujumla huku akitoa wito wa kuachiwa huru kwa Bazoum na kudumishwa kwa utaratibu wa kikatiba.

Ufaransa ina takriban wanajeshi 1,500 katika taifa hilo la Afrika Magharibi, ambalo ni moja ya washirika wake wa mwisho katika eneo la Sahel, baada ya vikosi vyake kuondoka katika nchi jirani ya Mali mapema mwaka huu.