Macron kusimamia mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Lebanon
9 Agosti 2020Macron siku ya Alhamisi alikuwa kiongozi wa kwanza duniani kufanya ziara mjini Beirut baada ya mripuko uliotokea siku ya Jumanne na kuwaonya viongozi wa Lebanon kuwa wakati msaada wa kimataifa utapatikana mageuzi makubwa yanahitajika kutatua matatizo ya nchi hiyo.
Mripuko huo katika bandari ya mjini Beirut, ambao lawama zinaelekezwa katika shehena kubwa ya kemikali ya amonia naitreti iliyohifadhiwa na kuachwa kuoza kwa miaka kadhaa katika bohari, uliharibu eneo lote la kitongoji. Mripuko huo umeongeza hasira ya Walebanon wengi dhidi ya tabaka linaloongoza nchi hiyo linalodaiwa kujitumbukiza katika ufisadi na rushwa pamoja na upendeleo.
Macron anatarajia kwamba ahadi zitakazotolewa katika mkutano huo kwa njia ya vidio, utakaoanza mchana leo, utakuwa mchango thabiti na fedha hizo zitatumika kwa uwazi na kwa lengo lililokusudiwa.
Akizungumza mjini Beirut baada ya ziara yake siku ya Alhamis, Macron alisema kuwa mkutano huo una lengo la kutafuta fedha kutoka mataifa ya Ulaya , Marekani na mataifa ya eneo hilo linaloizunguka Lebanon kwa ajili ya madawa, huduma, chakula, na kuwapa makaazi watu walioathirika.
Haja ya mageuzi Lebanon
"Pia tutaweka uongozi wa wazi na sahihi ili misaada hii yote , iwapo inatoka Ufaransa ama ya kimataifa, iweze kwenda moja kwa moja kwa watu, katika asasi za kijamii na timu katika maeneo ambayo yana uhitaji, bila ya uwezekano wa kuhodhi ama kupelekwa mahali ambako hakustahili," alisema.
Amesema kwamba haja ya mageuzi makubwa yanamaana "muda umewadia sasa wa uwajibikaji kwa Lebanon ya leo na viongozi wake" ambao wanahitaji " makubaliano mapya na watu wa Lebanon katika wiki zijazo."
Waziri mkuu Hassan Diab amesema siku ya Jumamosi kuwa ataitisha uchaguzi wa mapema.
Trump akithibitisha kushiriki kwake katika mkutano huo, aliandika katika ukurasa wa Twitter kuwa "kila mmoja anataka kusaidia!"
Chanzo katika ofisi ya rais ya Ufaransa ambacho hakikutaka kutajwa jina , kimesema kuwa Umoja wa Ulaya, Uingereza, China, Urusi, Jordan na Misri zitawakilishwa, licha ya kuwa haikufahamika mara moja katika ngazi gani. Israel, ambayo Lebanon haina uhusiano wa kidiplomasia nayo, haitarajiwi kushiriki.
Mataifa muhimu ya Kirabu katika eneo la ghuba, ikiwa ni pamoja na saudi Arabia, Qatar na Umoja wa falme za Kiarabu yanatarajiwa kushiriki lakini Iran, ambayo ina ushawishi mkubwa katika Lebanon kupitia kundi la Kishia la Hezbollah, haijaonesha nia ya kushiriki, afisa huyo alisema.